Na Queen Lema, Timesmajira Online, Arusha
Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimeishauri Serikali kuanzisha chombo maalum kitakachowawezesha wananchi kuwasilisha na kufuatilia malalamiko yao, hususani yanayohusu haki za binadamu na utawala bora.
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa mkutano mkuu wa TLS,Rais wa chama hicho Boniface Mwabukusi,amesema chombo hicho kinapaswa kuwa na mamlaka kamili, uhuru wa kiutendaji na uwezo wa kutoa maelekezo yenye uzito sawa na amri za mahakama.
“Kwa kuzingatia hali halisi ya utendaji kazi wa vyombo vya utoaji haki hususani Jeshi la Polisi na mazingira ya kiusalama kwa raia,kukithiri vitendo vya utekaji na kupotezwa kwa wananchi,TLS tunatoa rai kwa serikali kuunda chombo maalum cha kisheria kitakacho simamia na kuangalia namna ambavyo wananchi wanatendewa haki,”.
Amesema kuwa,mkutano huo unaongozwa na kauli mbiu isemayo “Uchaguzi na utawala wa sheria :wito wa uangalizi wa kisheria na uwajibikaji katika mfumo wa uchaguzi wa Tanzania”.
Ambapo amebainisha kuwa kauli mbiu hiyo inasisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa misingi ya utawala wa kisheria inazingatiwa katika kila hatua ya mchakato wa uchaguzi, kuanzia maandalizi ,upigaji kura hadi utoaji wa matokeo.Inafanya watafakari wajibu wao kama wanasheria na viongozi wa kitaaluma katika kulinda haki ya wananchi ,kudumisha amani na kuimarisha demokrasia.
“Katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, tunakumbushana kuwa uangalizi wa kisheria si hiari bali ni wajibu,uwajibikaji na msingi wa uongozi bora ,TLS tunaamini kwa kushirikiana na Serikali ,Mahakama , Tume Huru ya Uchaguzi ,vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi,tunaweza kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa haki,huru na kuaminika,”.
Pia amesema,wanatambua kwamba wanasheria wanao wajibu wa kulinda haki ya wananchi na kutetea misingi ya katiba ya nchi hasa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu.Pamoja na kuwa na wajibu wa kulinda utawala wa sheria,kushirikiana na serikali katika masuala ya kisheria yanayolenga ustawi wa jamii na ushiriki wao .
Akifungua mkutano huo Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti,Utumishi wa Umma na Utawala bora, George Simbachawene,amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya vyama vya siasa, taasisi za kisheria,huku akisisitiza kuwa TLS Ina mchango katika masuala ya kisheria na utawala bora, na ni chama muhimu katika kutoa miongozo ya kisheria na kuhamasisha demokrasia.
Simbachawene amesema ni muhimu kuzingatia maoni ya wananchi katika mabadiliko ya katiba na sheria ambapo alikubalina na mawazo ya kuboresha siasa nchini na kuahidi kushirikiana na TLS katika juhudi za kuboresha mifumo ya kisheria na utawala bora.
More Stories
TAKUKURU yanasa watuhumiwa wa wizi wa mali za wakulima
CCM yampongeza Rais Samia kutunukiwa tuzo na Bunge
Mwenge wazindua Miradi saba Temeke