Na Penina Malundo,Timesmajjira
MTANDAO wa Vijana na Wanawake unaoendesha vuguvugu la kujitolea ili kuleta mapinduzi kifikra kwa jamii (TK MOVEMENT ) mkoa wa Kagera imeungana na watanzania wengine nchini katika kusherekea siku ya kumbukizi ya kuzaliwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan huku wakimpongeza kwa mabadiliko makubwa na maendeleo yanayoendelea kufanyika chini kupitia sekta mbalimbali.
Akizungumza jana mkoani Kagera,Mratibu wa TK MOVEMENT mkoani humo,Chaelisious Charles wakati wa kusherekea siku hiyo ya kuzaliwa kwa Rais Samia na watoto yatima wa kituo cha Ntoma,mkoani humo,alisema mtandao huo umeamua kuadhimisha siku hiyo kwa kujumuika na watoto hao yatima kutokana na kuenzi upendo wa Rais Samia kwa watoto.
Amesema uongozi wa Rais Samia umejaa upendo, huruma na kujali ustawi wa kila Mtanzania, hususan watoto ambao ni hazina ya taifa letu.
”Tumekuwa tukishuhudia nukuu mbalimbali za Rais Samia ambazo zimekuwa zikitufundisha ikiwemo hii ya “Tuwalee watoto wetu kwa upendo, kwa sababu wao ndio taifa la kesho.” Ndiyo maana sisi kama TK Movement Mkoa wa Kagera, tumeona ni vyema kusherehekea siku hii kwa njia ya kuwafariji na kushiriki nanyi, tukiwakumbusha kuwa hata kama mama zenu hawapo, bado mna Mama wa Taifa – Mama Samia – anayewapenda, kuwaenzi na kuwatakia maisha bora,”amesema.
Amesema jamii ya Kagera inashuhudia mabadiliko makubwa na maendeleo yanayoendelea kufanyika chini ya uongozi wake mahiri ikiwemo uwepo wa miradi ya miundombinu, sekta ya elimu, afya, na uwezeshaji wa vijana na wanawake, yote haya ni matunda ya uongozi makini na wa kimaono wa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
”Sisi wana TK Movement Mkoa wa Kagera, kwa kauli moja, tunasema mwaka huu wa 2025 tuna deni kubwa kwake,tumejipanga kuhakikisha ushindi wa kishindo katika uchaguzi ujao, kwa sababu mambo aliyoyafanya yanajieleza yenyewe,”amesema na kuongezaÂ
”Tunatambua jitihada zinazofanywa na viongozi wetu wa Mkoa wa Kagera, wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Hajat Fatma Mwassa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Wabunge, Madiwani na viongozi wengine wote, ambao wamekuwa mstari wa mbele kueleza na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) chini ya uongozi wa Mama yetu, Dkt. Samia,”amesema.
Amesema TK Movement ni mtandao thabiti unaowaunganisha vijana,wanawake na makundi mbalimbali ya kijamii kwa ajili ya ukombozi wa kifikra, ukombozi wa kiuchumi na kuwaunganisha wananchi na fursa zilizopo katika maeneo yao.
”Tunaamini katika misingi ya Utaifa, Uzalendo na Kujitolea, Kauli mbiu yetu, “Mama yetu, Taifa letu,” inaakisi imani yetu kwa Mheshimiwa Rais na dhamira yetu ya kushirikiana naye katika kuijenga Tanzania yenye ustawi,”amesema.
Ameiomba jamii kuendelee kuwa wamoja, kupendana na kushirikiana katika kila jambo na kupitia kumbukumbu hii ya kuzaliwa kwa Rais Samia iwe chachu ya upendo na mshikamano zaidi kwa ajili ya watoto ,jamii na kwa ajili ya taifa.Â
More Stories
THBUB yatoa tamko kulaani mauaji ya Jumanne Juma
Dkt. Biteko aongoza waombolezaji kuaga miili ya wanafunzi waliofariki Geita
Bungua mweusi anayeshambulia zao la kahawa aibuka Bukoba