
Na Joyce Kasiki, Geita
MAMLAKA ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imetangaza fursa mbalimbali za uwekezaji katika sekta ya madini na nyinginezo, huku ikiwasilisha huduma kwa wawekezaji wanaoshiriki Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea jijini Geita.
Akizungumza leo, Oktoba 1, 2026, katika maonesho hayo yanayofanyika katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Geita, Mjumbe wa Bodi ya TISEZA, Absolom Kibanda, amesema ushiriki wa taasisi hiyo unalenga kutoa elimu kuhusu uwekezaji, kutangaza fursa zilizopo nchini na kuwasaidia wawekezaji kupata huduma zinazohitajika.
Kibanda amesema uwekezaji ni miongoni mwa nguzo muhimu katika kukuza uchumi wa taifa, akieleza kuwa TISEZA ina jukumu la kuhakikisha wawekezaji wa ndani na nje wanapata taarifa na huduma zinazowawezesha kutekeleza miradi yao.
Amesema Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa uwekezaji katika kukuza uchumi, kupitia sera na mikakati mbalimbali, hivyo wadau wa sekta ya umma na binafsi wanapaswa kushirikiana katika kutekeleza malengo ya maendeleo ya Taifa.
“Tunapozungumzia uwekezaji, tunazungumzia hatima ya taifa kiuchumi. Ni jukumu letu kufanya kazi kwa karibu ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa katika dira ya taifa yanafikiwa,” amesema Kibanda.
Kwa upande wake, Meneja wa TISEZA Kanda ya Ziwa, Venance Mashiba, amesema ushiriki wa mamlaka hiyo katika maonesho hayo una malengo makuu manne ambayo ni kutoa elimu kwa wananchi na wawekezaji, kuitangaza TISEZA, kutangaza fursa za uwekezaji na kutoa huduma kwa wawekezaji.
Amesema TISEZA ni taasisi mpya iliyoundwa baada ya kuunganishwa kwa Tanzania Investment Centre (TIC) na Export Processing Zones Authority (EPZA), hivyo maonesho hayo yametumika pia kuwafahamisha wananchi kuhusu majukumu ya taasisi hiyo.
“Tunatumia fursa hii kuitangaza taasisi ili watu waweze kuifahamu, lakini pia kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo katika eneo letu na nchini kwa ujumla,” amesema Mashiba.
Amesema TISEZA pia imewaleta pamoja baadhi ya taasisi zinazohusika na huduma kwa wawekezaji, ikiwamo Tanzania Medicines and Medical Devices Authority (TMDA), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Kwa mujibu wa Mashiba, hatua hiyo inamwezesha mwekezaji anayefika katika banda la TISEZA kupata ushauri na kufuatilia changamoto mbalimbali zinazohusu uwekezaji bila kulazimika kutafuta huduma hizo katika maeneo tofauti.
Amesema huduma hizo zinawahusu wawekezaji wakubwa na wadogo katika sekta mbalimbali, huku TISEZA ikiwa na jukumu la kutoa taarifa kuhusu fursa za uwekezaji na kuwaunganisha wawekezaji na taasisi husika.
Kuhusu wachimbaji wadogo wa madini, Mashiba amesema TISEZA inaweza kutoa taarifa na huduma kwa wawekezaji wanaohitaji kuwekeza katika sekta ya madini, ingawa baadhi ya huduma zinazohusu shughuli za uchimbaji wa madini zinasimamiwa moja kwa moja na Wizara ya Madini.
Amesema TISEZA huanza kushirikiana zaidi na mwekezaji pale shughuli ya uwekezaji inapofikia hatua zinazohitaji huduma za uwekezaji, ikiwamo taarifa, vibali, uwezeshaji na vivutio vinavyotolewa na Serikali.
Mashiba amesema mamlaka hiyo pia inaendelea kutumia semina, makongamano na warsha kuwaelimisha wawekezaji kuhusu fursa zilizopo katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema TISEZA inatarajia kuendesha semina maalumu mkoani Geita zitakazolenga zaidi wawekezaji wa sekta ya madini, kwa lengo la kuwapa taarifa kuhusu fursa zilizopo katika mnyororo mzima wa thamani wa madini.
Ameongeza kuwa baadhi ya changamoto ambazo wawekezaji wameziwasilisha katika banda la TISEZA wakati wa maonesho hayo zinahusu vibali vya ukaazi, masuala ya ardhi na taratibu mbalimbali zinazohusiana na uwekezaji.
Kwa upande wa fursa za uwekezaji Kanda ya Ziwa, Mashiba amesema zipo katika maeneo mbalimbali, huku akitaja sekta ya madini mkoani Geita na maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji kuwa miongoni mwa fursa zinazoweza kuendelezwa.
Amesema eneo la Buzwagi lililopo Kahama, mkoani Shinyanga, limetengwa kwa ajili ya uwekezaji na TISEZA inaendelea kuhamasisha wawekezaji kutumia fursa hiyo kuanzisha viwanda na miradi mingine ya uzalishaji.
Amesema Geita ni miongoni mwa maeneo muhimu kiuchumi Kanda ya Ziwa kutokana na shughuli kubwa za madini, jambo linaloifanya mkoa huo kuwa eneo muhimu katika kuhamasisha uwekezaji unaohusiana na sekta hiyo.
Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanaendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Geita, yakishirikisha wadau mbalimbali wa sekta ya madini, teknolojia, uwekezaji na biashara.

More Stories
UWT yahimizwa kusimamia malezi bora
Uwekezaji wa Michezo wavutia Watalii Tanzania
Mkurugenzi Bonde Rufiji, ahimiza utunzaji vyanzo vya maji