Na Sophia Fundi, Timesmajira Online, Karatu
TIMU ya mpira wa miguu Tiger FC, kutoka tarafa ya Eyasi Mangola wilayani Karatu mkoani Arusha, imejinyakulia kombe la Karatu Super Cup baada ya kuibuka na ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Young Beach kutoka Karatu mjini katika mchezo wa fainali uliochezwa juzi kwenye viwanja vya Mnadani wilayani hapa.
Mchezo huo ambao ulishirikisha timu 76 kutoka kata 14 za Wilaya hiyo, ulikuwa na ushindani wa hali ya juu licha ya mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo kumalizika, mdhamini wa Karatu Super Cup, wakili Samweli Welwel amewaomba wadau wa mchezo wilayani hapo kushirikiana katika kuhakikisha Karatu inakua kimichezo na kuwainua vijana kupitia sekta hiyo.
Welwel amesema, Karatu ni yetu sote hatuna budi kushikamana katika kuendeleza mchezo kwa ngazi zote ambapo aliwaomba wadau kutohusisha siasa kwenye mchezo.
“Ligi hii ya Karatu Super Cup pamoja na kuwa nimedhamini Mimi Mwenyekiti wa Chadema Wilaya, nilipata ushirikiano kutoka kwa mbunge wa Jimbo la Karatu Daniel Awack katika kuendeleza hivyo nawaomba wanakaratu tuendelee kushirikiana tupate timu hata moja ambayo itakuwa mfano kwa Wilaya zingine”amesema Welwel.
Amesema, tayari amesaini mkataba wa miaka mitatu na chama Cha soka wilaya ya Karatu ya kudhamini Karatu Supar Cup, hivyo anaomba ushirikiano na wadau wa michezo wilayani humo.
Kwa upande wake mwenyekiti wa soka Wilaya ya Karatu, John Marmo amemshukuru mdhamini wa mashindano hayo Kwa hatua walikofikia ya fainali na kumpata mshindi, kwani ni mashindano ya kihistoria Wilayani Karatu kushiriki timu nyingi katika kumtafuta mshindi.
“Tunakushukuru Welwel, kwani katika kumtafuta mshindi tulianzia ngazi ya chini kwa timu 72 kushiriki hadi kufikia leo, tunahitimisha fainali na haijawahi Kwa Karatu timu nyingi kushiriki namna hii tunaomba wadau tuendelee kudhamini mashindano katika Wilaya yetu,”amesema John.
Mwenyekiti wa mpira wa miguu mkoa wa Arusha, Zakayo Mjema amewataka wanamichezo kuwa na nidhamu ya mpira ili wadhamini kuendelea kudhamini mashindano mbalimbali katika ngazi zote.
Amewaomba wanaKaratu, kuungana kutafuta timu moja ambayo itawakilisha Karatu katika ligi mbalimbali nje ya Wilaya.
Katika mchezo huo mshindi wa Kwanza Timu ya Tiger Fc kutoka Mangola ilipewa zawadi ya sh.milioni moja na elfu kumi pamoja na seti ya jezi na kupata nafasi ya kwenda ziara ya mbuga yeyote ya wanyama kutembelea, wakifuatiwa na Young Beach aliyepewa zawadi ya shilingi laki Saba na seti ya Jezi.
More Stories
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Rais Samia: Yanga endeleeni kuipeperusha bendera ya Tanzania