December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TIC, washirika kujiridhisha miradi inavyoibua ajira, kuchangia ukuaji uchumi

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online Dodoma

KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na taasisi 12 zinazoshirikiana na kituo hicho jana zimeazimia kutembelea miradi ambayo imepitishwa na TIC kujiridhisha juu ya namna miradi hiyo inavyoibua ajira na kuchangia katika ukuaji wa pato la Taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza kikao cha TIC na taasisi hizo 12 kilichofanyika katika Ofisi za Waziri Mkuu Jijini hapa, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Dkt. Maduhu Kazi, amesema kikao hicho ni sehemu ya mwendelezo wa vikao vyenye lengo la kujadili changamoto na kuibua mapendekezo yatakayosaidia kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.

“Tumeazimia kuanza kutembelea miradi mbalimbali ambayo imepitishwa na TIC ambayo sote tulishirikiana kuipitisha kwa kutumia kwa kutumia chengo yetu ya huduma ya mahala ya pamoja (one stop facilitation centre) ili kujionea maendeleo ya miradi hiyo na namna inavyochangia katika kuzalisha ajira na kukuza pato la taifa,” amesema Dkt.Kazi

Amesema moja ya miradi itakayotembelewa ni pamoja na kiwanda cha kutengeneza mbolea ya asili cha Intracom Limited ambacho pia kilitembeliwa jana.

Kiwanda hicho kinajengwa Nala jijini hapa na ambocho kimepewa cheti cha uwekezaji namba 20214355 kupitia chengo ya huduma mahala pamoja.

“Wakuu wa taasisi watakitembelea kiwanda hiki na kujionea maendeleo ya mradi huo ambao unatarajiwa kutekelezwa kwa muda wa miaka mitatu hadi 2024 ambapo kwa sasa mradi huu umefikia asilimia 52 ya utekelezaji wake,” amesema Dkt.Kazi

Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya kuhamasisha Uwekezaji(NIFC) Dkt. Maduhu Kazi (katikati) akizungumza kwenye kikao cha kamati hiyo kilichowakutanisha Wakuu wa Taasisi zinazounda huduma ya mahala pamoja (One Stop Facilitation Centre) kujadili namna bora ya kuboresha huduma za uwekezaji ili kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara kuwekeza hapa nchini. Kikao hicho kilifanyika katika Ofisi za Waziri Mkuu Jijini Dodoma jana. Na mpiga picha wetu.

Ameeleza kuwa kampuni hiyo imewekeza zaidi ya dola za Marekani milioni 180 na kwamba inatarajiwa zaidi ya ajira za moja kwa moja zaidi ya 3000 zataibuliwa na zisizokuwa za moja kwa moja ni 1500. Zaidi ya tani laki sita (600,000) zitazalishwa kila mwaka.

“Mradi huu utalifanya eneo la viwanda la Nala kuchangamka kimaendeleo na kupelekea kuzalishwa kwa fursa mbalimbali za ujasiriamali jambo litakalopelekea wananchi wengi kujiajiri na wengine kuajiriwa,” amefafanua Dkt.Kazi.

Ameeleza kuwa kukamilika kwa kiwanda hicho kutatoa fursa kwa Watanzania kuuza malighafi mbalimbali katika kiwanda hicho ili kuzalishe mbolea ambayo inahitajika kuendeleza kilimo nchini.

“Malighafi za samadi na phosphate zitahitajika kutengeneza mbolea ambayo ni ya asili. Hivyo kutakuwa na vituo vya ukusanyaji nchini kote ili kurahisisha upatikanaji wa malighafi hiyo na kwa njia hiyo kutoa fursa ya biashara kwa wafugaji wakubwa na wadogo hapa nchini,” amesema Dkt.Kazi

Naye mjumbe wa kamati hiyo ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara(TNBC), Dkt. Godwill Wanga, amesema jambo umuhimu ni kuhakikisha mfumo wa pamoja wa kuwahudumia wawekezaji unajengwa ili kutoa fursa kwa wawekezaji kupata huduma kwa haraka, wawekeze na kuiletea nchi faida.

“Tunapokuwa kwenye mfumo mmoja kama taasisi za kuhudumia wawekezaji na wafanyabiashara ufanisi katika usajili miradi utaongezeka pamoja na kuwafanya wawekezaji zaidi kuja kuwekeza hapa nchini,” amesema Dkt.Wanga

Dkt Kazi ameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara na kufafanua kuwa uboreshaji huo umeongeza idadi ya wawekezaji nchini. Amesema mwaka jana Rais Samia Hassan ametembelea Burundi na kwamba ujenzi wa kiwanda cha mbolea ni matokeo ya ziara hiyo.