November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TIA, GEL zasaini mkataba kutafuta fursa nje ya nchi

Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa elimu nje ya nchi Global Education Link (GEL) Abdulmalik Mollel kushoto akibadilishana nyaraka na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Profesa William Pallangyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa elimu nje ya nchi Global Education Link (GEL) Abdulmalik Mollel, Kushoto na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Profesa William Pallangyo (kulia) wakionyesha mkataba waliosaini jana kwenye ofisi za GEL Chang’ombe jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa elimu nje ya nchi Global Education Link (GEL) Abdulmalik Mollel, Kushoto akisaini mkataba na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Profesa William Pallangyo (kulia) kwenye ofisi za GEL Chang’ombe jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online DSM

TAASISI ya Uhasibu Tanzania (TIA), imesaini mkataba na wakala wa vyuo vikuu nje ya nchi Global Education Link (GEL), lengo ikiwa ni kushirikiana kuitafutia taasisi hiyo fursa za wanafunzi na wahadhiri kwenye vyuo vikuu vya nje.

Mkataba huo umesainiwa kwenye ofisi za GEL Chang’ombe jijini Dar es Salaam, baina ya Mkurugenzi Mtendaji wa wakala, Abdulmalick Mollel na Ofisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Profesa William Pallangyo.

Akizungumza mara baada ya kusaini mkataba huo, Mollel amesema GEL kwa miaka 16 imekuwa ikisaidia watanzania wanaotaka kwenda kusoma nje ya nchi kuanzia ngazi ya Cheti, Stashahada, Shahada, Shahada za Uzamili na za Uzamivu ili kutimiza ndoto zao kwenye taaluma wanazozipenda.

Amesema jukumu lingine la GEL ni kuishauri serikali inapoona fursa zilizoko nje ya nchi ambazo haziko hapa nchini namna watanzania wanavyoweza kunufaika na fursa hizo.

Mollel amesema wamekuwa wakisaidia kutengeneza ushirikiano kati ya vyuo vikuu vya nje ya nchi na vya ndani ya nchi na kwamba kabla ya kufanya hivyo lazima GEL iwe na makubaliano na chuo kinachotaka kuunganishwa na vyuo vya nje zaidi ya 300 wanavyofanyakazi navyo.

Amesema GEL itashirikiana na TIA kupata mikataba yenye tija na vyuo vikuu vya nje kuanzia kwenye kupata ufadhili wa masomo kwa wahadhiri wake kwenda kusoma ngazi ya Shahada za Uzamili au za Uzamivu.

“Tunatamani kuona vyuo vikuu vyetu vinakuwa na kozi ambazo zinaweza kushirikiana na vyuo vya nje kwa kusoma miaka miwili hapa nchini na kwenda kumaliza kwenye vyuo vya nje kwa kutumia mitaala ya hapa nchini au mitaala ya nje ya nchi na hii itasaidia sana sisi kupata wanafunzi wa kimataifa kuja kusoma hapa kwetu,” amesema Mollel

Amesema vyuo vikuu vingi duniani vinafanya mikutano ya kimataifa ambapo wahadhiri wa vyuo vya ndani wanaweza kushirikiana na wahadhiri wa vyuo hivyo kutoa machapisho mbalimbali kwa pamoja na kutoa mafunzo ya pamoja kwa wanafunzi wa vyuo vyao.

Amesema mikataba kama hiyo itasaidia kuvitambulisha vyuo vikuu vya hapa nchini kwenye mataifa mbalimbali ili wanafunzi wa nchi hizo wajue kozi zinazotolewa na kuja kusoma hapa nchini.

“Leo hii kuna maonyesho ya vyuo vikuu zaidi ya 200 nchini China ambavyo vina fursa za kutosha kwa hiyo vyuo vikuu vyetu navyo vinapaswa kushiriki maonyesho kama haya kuvutia raia wa mataifa hayo waje kusoma kwenye vyuo vyetu hapa,” amesema

Amesema vile vile mkataba huo utakiwezesha chuo hicho kubadilishana wanafunzi na vyuo vikuu vya nje kwa wanafunzi wake kusoma hapa nchini nusu ya muhula na kwenda kumalizia nje ya nchi na wale wa nje ya nchi kuja kumaliza muhula wao hapa nchini.

Amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameitangaza Tanzania kimataifa na kuvutia uwekezaji mbalimbali ambapo wengine wamewekeza kwenye teknolojia ya kisasa hivyo kuna umuhimu wa vijana wa Tanzania kwenda kusoma masuala ya teknolojia na kuja kufanyakazi na wawekezaji hao.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa (TIA), Profesa William Pallanyo, amesema mwaka huu TIA inafikisha miaka 50 ikiwa inafunisha masomo ya uhasibu, rasilimali watu, ununuzi, masoko kwenye kampasi sita za Dar es Salaam, Singida, Mwanza, Mbeya, Kigoma na Mtwara na kwamba mwakani wanatarajia kuanzisha kampasi visiwani Zanzibar.

Amesema GEL imekuwa ikiwasaidia wanafunzi wa Tanzania kupata vyuo vya kujiendeleza nje ya nchi hivyo kuingia mkataba nayo kutatoa fursa kubwa kwa TIA kutoa mafunzo ya kimataifa kwa wanafunzi wa chuo hicho kupata nafasi ya mafunzo kwenye vyuo ambavyo watashirikiana kupitia GEL.

“MoU hii ni fursa nzuri kwa wanafunzi na wahadhiri wetu kupata vyuo vikuu vya kujiendeleza nje ya nchi ka wale wanaotaka kusomea Shahada za Uzamili na Shahada za Uzamivu na tutapata fursa ya kupata machapisho kwenye maktaba za wenzetu nje ya nchi,” amesema Profesa Pallangyo.

“Hii itawapa fursa vijana wetu kukua kadri teknolojia inavyozidi kukua duniani kwasababu teknolojia inabadilika kwa haraka sana kwa hiyo tukiendelea kujifungia ndani uwezekano wa kwenda na kasi ya wenzetu tutakuwa tumechelewa, baada ya kusaini hapa tutaanza kufanya yale yote yaliyotajwa kwenye mkataba huu,” amesema Profesa