Na Judith Ferdinand, Mwanza
CHAMA cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania ((THTU) kimeiomba Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu
iendelee kuboresha changamoto za kisheria, kisera zinazopelekea
mazingira magumu na kuongeza mzigo kwa wafanyakazi wa
Taasisi za Elimu ya Juu.
Hayo yalizungumzwa na Kaimu Katibu Mkuu wa THTU Elia Kasalile kwenye ufunguzi wa mkutano mkuu wa sita(maalum) wa chama hicho uliofanyika mkoani Mwanza ambapo wanachama takribani 120 wa chama hicho walipata fursa ya kushiriki huku kauli mbiu ya chama hicho ikiwa ‘Nia na mwelekeo wetu daima ni kujenga taifa kwanza’.
Kasalile amesema,kwa kufanya hivyo kutapelekea kupata sheria
na sera zinazoendana na wakati na zinazokidhi mahitaji ya
watumishi kwa ujumla wake hali itakayoongeza chachu ya kufanya
kazi na kukua kwa utoaji wa huduma bora kwa umma.
“Chama kinaendelea kutoa rai kwa Serikali pamoja na mamlaka zake kwa ujumla kuendelea kuboresha sheria, sera na taratibu
mbalimbali ili kupunguza changamoto zinazowakabili watumishi
katika maeneo yao ya kazi,kwani,uwepo wa sera na sheria
zinazohamasisha mazingira mazuri ya kazi zitapunguza mzigo mkubwa kwa watumishi hali itakayopelekea kuongeza ufanisi pamoja na utendaji bora mahala pa kazi,” amesema Kasalile.
Kwa upande wake Mwenyekiti Taifa wa THTU Dkt.Paul Loisulie, alimuomba Mkuu wa Mkoa wa Mwanza awafikishie ujumbe kwa rais kuwa menejimenti ya taasisi iache kuingilia majukumu ya vyama vya wafanyakazi,kwani unakuta menejimenti hizo zinataka ziwekee mwakilishi kwenye vyama hivyo.
Loisulie amesema,taasisi za Serikali zitoe ushirikiano wa ziada pale vyama vya wafanyakazi wanapoenda kuongea nao na kujadiliana masuala yanayohusu maslahi ya wafanyakazi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella ambaye alikua mgeni rasmi katika mkutano huo amesema,sekta hiyo ni nyeti hivyo katiba yao inatakiwa iwe itakayofanya chama hicho kuwa imara zaidi na kutoa mchango mkubwa kwa taasisi wanazotoka na taifa kwa ujumla.
Mongella amesema, taasisi za elimu ya juu bado zimejitenga na jamii,hivyo vyuo vinapaswa kushuka hadi chini kwa jamii ili kuipatia mawazo mapya ya kimaendeleo pamoja na kufanya juhudi za kuelimisha viongozi ambao watafikisha elimu hiyo kwa wananchi pamoja na kuanzisha mafunzo hata ya muda mfupi kwa viongozi ili kuwajengea uwezo zaidi.
“Taasisi za elimu ya juu mjitahidi kuzalisha vijana wachapakazi waliopata mafunzo kwa vitendo ambao wanakuja kutoa majawabu ya changamoto yanayowakabili sehemu zao za kazi,” amesema Mongella.
Hata hivyo mmoja wa washiriki wa mkutano huo, Mwenyekiti wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDASA) Dkt. George Kahangwa, amesema shida na changamoto zinazowagusa wafanyakazi siyo tu wa vyuo vikuu ila za wafanyakazi wote ziondoke.
“Kwani kipindi hiki sisi tunazungumza wafanyakazi yanayotuhusu lakini wapo ambao wanaomba kazi katika kipindi hiki ambao katika kuomba kwao wanasema mmenielewa na sisi tunaomba watuelewe na tuelewane ambapo katika utekelezaji lazima tupate uwezesho na haki zetu na tupate mazingira mazingira mazuri kwani wenye njaa wanazalisha kidogo wakifa moyo kiwango chao kinashuka,” amesema.
More Stories
Wananchi Kisondela waishukuru serikali ujenzi shule ya ufundi ya Amali
RC.Makongoro ataka miradi itekelezwe kwa viwango
LALJI yatoa msaada wa sare na vifaa vya shule kwa yatima