November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

THRDC yaguswa na mashirika yasiyo ya kiserikali kufutwa

Na Penina Malundo,timesmajira 

MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umesema kuwa umeguswa na kufutwa kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali  (AZISE) 4,898 kwa maelezo kuwa yamekiuka sheria, kanuni na miongozo inayosimamisha shughuli za mashirika hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Wakili wa Mtandao huo, Paul Kisabo amesema idadi hiyo ya mashirika yaliyofutwa ni kubwa kuwahi kutokea katika historia ya nchi na kwamba kama mtandao wameona ni vyema kufuatilia suala hilo ili kubaini changamoto ambazo mashirika yanakumbana nazo na kuona ni kwa namna gani kwa pamoja watazifanyia kazi.

Amesema mtandao huo umeguswa na jambo hilo kwa sababu ni shirika huru la wanachama lenye jumla ya mashirika yasiyo ya kiserikali 250 nchini Tanzania ambao asilimia 10 ya wanachama wa THRDC ni wahanga wa jambo hilo.

“Tumeguswa na jambo hili kwa sababu mojawapo la jukumu kuu la THRDC ni kufuatilia na kutetea mazingira wezeshi ya watetezi wa haki za binadamu na nafasi za kiraia hapa nchini. Katika kutekeleza jukumu hili THRDC imekuwa ikipitia wakati mgumu lakini tunashukuru kwa Rais Samia Suluhu ameweka wazi kuwa watetezi wa haki za binadamu tufanye kazi zetu kwa uhuru na tuzungumze na serikali yake na watendaji wake pale ambapo tumeona mambo hayapo sawa,” amesema Wakili Kisabo 

Kisabo amesema pamoja na kuguswa na hilo, mtandao umejiridhisha kuwa taratibu zote za kisheria zimezingatiwa katika ufutwaji wa mashirika haya ikiwemo kupewa nafasi za kujitetea. 

“Kwa kupitia utafiti wa Mfumo wa NIS-Jamii, THRDC, NACONGO pamoja na ofisi ya msajili tulibaini kweli yapo mashirika mengi yasiyowasilisha taarifa za mwaka na kulipa ada za mwaka. Lakini pia utafiti huu pamoja na takwimu za Ofisi ya Msajili zinaonyesha mashirika mengi , karibu asilimia 30 ya zilizosajiliwa hazitumii mfumo wa NIS-Jamii. Wakati huo huo mashirika mengi takribani asilimia 50 ya mashirika yaliyosajiliwa hayatoi taarifa za mwaka na kulipa ada,” amesema Wakili Kisabo

Amesema kama mtandao hawana tatizo na mashirika yaliyofutwa kwa kukiuka sheria endapo kama yalisikilizwa kikamilifu kwa mujibu wa sheria na Katiba ya Tanzania na kwamba kutokana na ukubwa wa tatizo la AZISE kutokutimiza masharti ya kisheria huenda yangefutwa mengi zaidi ya hayo.

Hata hivyo Wakili Kisabo amesema moja ya sababu ya mashirika hayo kufutwa ni kutokana na kwamba mengi hayana fedha za kujiendesha yenyewe hivyo inasababisha yanashindwa kufanya kazi au wakati mwingine mengi yamekuwa yakifanya kazi kwa kujitolea. 

“Hii husababisha mashirika kufikia hadi mwisho wa mwaka bila ya kuwa na ripoti ya kuwasilisha kwa msajili au ada ya kulipa hivyo kudhaniwa kuwa yanakiuka sheria kwa makusudi. Lakini pia wafanyakazi hufanya kazi kwa kujitolea katika mashirika mengi bado hawajui hata kama hawajapata fedha wanaweza kupeleka taarifa kwa msajili wa kile walichokifanya,” amesema

Naye Ofisa Uchechemuzi wa THRDC, Nuru Maro ameyataka mashirika kuendelea kuzingatia matakwa ya kisheria na kikanuni kwa sasa ili kuepuka kuingia kwenye hatari ya kusimamishwa kufanya kazi au kufutwa kabisa pamoja na kuendelea kushirikiana na Serikali katika kufanya kazi ili kuleta maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kiutamadauni.

“Tunamuomba msajili na serikali kwa ujumla kuandaa takwimu zinazoonyesha hali ya ufadhili kwa mashirika ya ndani hapa nchini, kushawishi wafadhili kujengea uwezo mashirika ya ndani kwa kuwapa rasilimali za kutosha zinazoweza kufanya wawe na uwezo kama mashirika mengine,” amesema Maro