January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

THBUB Kutembelea Mikoa 24 kufuatilia malalamiko

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora(THBUB),inatarajia kutembelea Mikoa 24 nchini ili kuzungungumza na viongozi wa ngazi mbalimbali wa Serikali, Asasi zisizo za kiserikali(AZAKI) na kufuatilia malalamiko 561 ya wananchi yaliyowasilishwa Tume.

Hayo yameelezwa jijini hapa leo na Kaimu Katibu Mtendaji wa THBUB,Nabor Assey wakati akizungumza  na waandishi wa habari kuhusu Tume hiyo kufanya mazungumzo na viongozi wa serikali na AZAKI mikoa 24 nchini.

Assey amesema lengo la ziara hiyo ni kuitambulisha Tume na majukumu yake ,kuimarisha uhusiano na ushirikiano katika utendaji kazi hususan katika ulinzi na ukuzaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora,kutafutia ufumbuzi malalamiko 561 ya wananchi na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya haki za binadamu na utawala bora.

“Katika ziara hii itaongozwa na Makamishna na Maafisa waandamizi,Tume itakutana na kufanya mazungumzo na wajumbe wa sekretarieti za mikoa 10 ambapo mikoa mitano Tanzania Bara na mitano Zanzibar,pia tume itakutana kuzungumza na viongozi na watendaji wa AZAKI takribani 82,”amesema.

Ametaja sekretarieti za mikoa ambazo Tume itakutana na kufanya mazungumzo nazo kwa upande wa Tanzania Bara ni Dodoma,Kigoma,Kagera,Tanga na Lindi na kwa upande wa Zanzibar ni Mjini Magharibi,Kaskazini Unguja,Kusini Unguja,Kaskazini Pemba na Kusini Pemba.

Mikoa mingine ni Dar es Salaam,Morogoro,Singida,Arusha,Mtwara,Ruvuma,Iringa,Mbeya,Songwe,Tabora,Shinyanga,Mwanza, Mara na Geita.

“Ziara hii inafanyika ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango mkakati wa THBUB wa  miaka mitano 2018/19-2022/23 ambao miongoni mwa malengo yake ni kulinda na kukuza haki za binadamu na misingi ya utawala bora,”amesema.

Amesema Tume inaamini kuwa ziara hiyo itasaidia viongozi,hususan wa serikali za Mitaa,AZAKI na wananchi wengi zaidi kuifahamu Tume,kazi zake na huduma inazozitoa.