April 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Katibu TSC awaasa walimu kutumia chombo chao kupeleleka malalamiko,kukata rufaa

Na Joyce Kasiki,Dodoma

KATIBU wa Tume ya Utumishi wa Walimu nchini (TSC) Paulina Mkwama amewataka walimu wote nchini walio katika Utumishi wa Umma  kukata rufaa katika Tume hiyo pindi wanapopewa adhabu kutokana na kufanya makosa mbalimbali ili rufaa hizo ziweze kushughulikiwa na siyo vinginevyo.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu majukumu ya TSC kwa njia ya mtandao  katibu huyo amesema kuwa mwalimu aliye katika Utumishi wa Umma anapoona hajaridhika na adhabu iliyotolewa na mamlaka yake ya nidhamu ngazi ya wilaya anapaswa kukata rufaa makao makuu ya TSC ambapo akiona bado hajaridhika anapaswa kukata rufaa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya walimu wanapoadhibiwa na mamlaka zao za nidhamu ,badala ya kukata rufaa na kwa kufuata taratibu zilizopo ,wanaenda kutoa malalamiko yao kwa vyombo ambavyo havihusiki nao.

“Kama mwalimu ameadhibiwa na mamlaka yake ya nidhamu ngazi ya wilaya anapaswa kukata rufaa Makao Makuu ya TSC ,lakini pia akiona bado hajaridhika na uamuzi uliotolewa na Makao Makuu anayo haki ya kuakata rufaa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na siyo kwenda kulalamika mahali popote anapoamua yeye.”amesema Mkwama

Aidha amesema,moja ya jukumu la TSC ni kuwasimamia walimu walio katika utumishi wa umma katika masuala mbalimbali yakiwemo ya kinidhamu huku akibainisha baadhi ya makosa ambayo yanaweza kumtia mwalimu hatiani kuwa ni pamoja na mwalimu kukataa uhamisho,mwalimu kutoripoti kazini,mwalimu kufanya vitendo vya ukatili kwa watoto,mwalimu kung’ang’ania kituo cha awali , mwalimu kushindwa kutekeleza majukumu aliyopewa na mwajiri wake pamona na  uzembe kazini .

Mkwama amesema,kwa mwalimu anayebainika kufanya makossa mbalimbali anaweza kupewa adhabu mbalimbali ikiwemo,kushushwa cheo,kushushwa mshahara ama kufukuzwa kazi.

Kiongozi huyo amezungumzia kuhusu maadili ya mwalimu huku akisema,mwalimu anapaswa kuwa katika haiba nzuri inayoendana na maadili ya ualimu katika mavazi na muonekano wake wa ujumla.