June 7, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TFS yawakaribisha wawekezaji katika vivutio vya utalii wa misitu

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira, Arusha

WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeeleza mikakati na fursa mbalimbali za uwekezaji na utalii wa misitu, huku ukizindua aina mpya ya vivutio ikiwemo usafiri wa waya (zipline) katika Ziwa Duluti, ikiwa ni sehemu ya kuongeza mazao na shughuli za utalii katika kampeni ya kuvutia watalii na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Akizungumza katika Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Karibu Kilifair 2025 yanayoendelea jijini Arusha Juni 6,2025, Yusuph Tango – Mhifadhi TFS, alisema lengo la kushiriki maonesho hayo ni kuwafikia wadau muhimu na kuwaeleza fursa zilizopo katika sekta ya utalii wa misitu nchini.

“Tuko hapa kuwaeleza wadau wetu kuhusu mazao ya utalii tuliyonayo. Tuna maeneo mengi ya misitu nchini yenye vivutio vya kipekee vinavyofaa kwa utalii wa kimazingira na pia tuna fursa nyingi za uwekezaji wa huduma kama vile malazi, burudani (recreations) ndani ya misitu,” alisema Tango.

Aliendelea kusema, TFS kwa kushirikiana na wadau imeanzisha mazao ya kipekee ikiwemo usafiri wa waya (zipline) katika Ziwa Duluti, Arusha, ambacho kitakuwa cha kwanza nchini kupita juu ya maji, jambo linalotoa fursa ya kumbukumbu za kipekee kwa watalii.

Kwa mujibu wa Tango, TFS imeweka mkazo katika kukuza utalii wa misitu kwa kushirikiana na sekta binafsi kuwekeza katika maeneo yenye vivutio vya asili, huku akibainisha kuwa baadhi ya misitu tayari imeanza kunufaika na uwekezaji huo.

Akitolea mfano wa matukio yanayotarajiwa mwezi huu wa Juni, Tango alieleza kuwa TFS inaandaa matukio mawili makubwa ya utalii wa mazingira — Rubare Marathon itakayofanyika ndani ya Shamba la Miti Rubare, Bukoba, na West Kili Forest Challenge itakayofanyika katika Shamba la Miti West Kilimanjaro, jirani na geti la Londorosi linaloelekea Mlima Kilimanjaro.

“Katika matukio haya kutakuwa na shughuli kama mbio za msituni, kuendesha baiskeli, mbio za pikipiki, pamoja na kutembelea maporomoko ya maji na vivutio vya kipekee ndani ya misitu,” alisema.

Mbali na hayo, TFS pia imetangaza kuongeza msukumo katika kukuza utalii wa nyuki (api-tourism), ambao umeanza kuonyeshwa kama zao jipya la kiutalii nchini. Kwa sasa, shughuli hiyo inatekelezwa katika maeneo ya Mlima Hanang, Vikindu (Mkuranga), na maeneo mengine yanayoratibiwa kuingizwa kwenye mpango huo.

“Mhe. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati walionesha kuvutiwa sana na api-tourism. Walituhimiza tuiendeleze maeneo mengine ili itoe tija kwa taifa na jamii zinazozunguka misitu hiyo,” alieleza Tango.

Amesisitiza kuwa TFS imejipanga kushiriki kikamilifu katika kufanikisha azma ya serikali ya kuongeza idadi ya watalii nchini, kwa mujibu wa malengo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala.

“Malengo ya serikali ni kuongeza watalii. Sisi TFS tumepewa jukumu la kuchangia hilo kupitia vivutio vya misitu na huduma bunifu za utalii. Kwa hiyo, tuko tayari kushirikiana na wadau wote kuifikia Tanzania ya utalii endelevu,” alihitimisha.

Maonesho ya Karibu Kilifair 2025 yanayofanyika jijini Arusha, yamekusanya wadau wa sekta ya utalii kutoka mataifa mbalimbali, ambapo TFS ni miongoni mwa taasisi za serikali zinazotumia jukwaa hilo kuhamasisha uwekezaji na kukuza utalii wa ndani.