March 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TFS yapanda Miti 1,500 Kuadhimisha Siku ya Misitu Duniani Tabora

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

Tabora. Jumla ya miche 1,500 ya miti imepandwa Wilaya ya Tabora Machi 21, 2025, katika maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani yaliyoandaliwa na Ofisi ya Mhifadhi Misitu (TFS).

Mhifadhi wa Misitu Wilaya ya Tabora, Aloyce Kilemwa, amesema kati ya miti hiyo, 154 imepandwa katika eneo la Tembe la Dr. Livingstone, Kwihara, huku miche mingine 1,346 ikigawiwa kwa wananchi, taasisi za serikali na binafsi ili kuhamasisha utunzaji wa mazingira.

Ametaja aina ya miti iliyopandwa kuwa ni Mkola (Afzelia quanzensis) 500, Mwerezi (Cedrela odorata) 300, Mtimaji (Trichilia emetica) 300, Mfududu (Gmelina arborea) 100, Mpera (Psidium guajava) 200, na Mpapai (Carica papaya) 50.

Mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Deusdedith Katwale, amepongeza juhudi za TFS katika kuhifadhi misitu na amewahimiza wananchi kutumia msimu huu wa mvua kupanda miti katika maeneo yao.

Aidha, ameelekeza TFS kuendelea kulinda hifadhi za misitu kwa uangalizi wa hali ya juu, kuhakikisha Hifadhi ya Igombe inalindwa kwa kuwa ni chanzo kikuu cha maji kwa wakazi wa Tabora, na kushirikiana na ofisi yake katika jitihada za utunzaji wa mazingira.

Zoezi hilo lilihudhuriwa na viongozi wa serikali, wakazi wa Tabora, na wadau wa mazingira walioungana katika kampeni ya upandaji miti kama hatua ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kulinda rasilimali za misitu kwa maendeleo endelevu.