November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TFS kuhakikisha nchi inapata bidhaa bora zitokanazo na zao la misitu

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Dar es Salaam

WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) itahakikisha nchi inapata bidhaa bora zitokanazo na zao la misitu pamoja na kuimarisha mifumo ya ikolojia nchini ili iweze kutoa hewa safi, maji na makazi bora ya wanayamapori.

Akizungumza jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari, baada ya kutembelea mabanda yaliyopo kwenye maonesho ya 47 ya Biashara Kimataifa Sabasaba Kamishina wa Uhifadhi wa TFS, Prof, Dos Santos Silayo, amesema TFS imepewa wajibu wa kuhakikisha nchi inapata bidhaa bora zitokanazo na zao la misitu.

Amesema zao la misitu ni muhimu ambalo hutumika kwenye maendeleo ya taifa kuanzia bidhaa za ujenzi, Nishati zinazotokana na mimea hiyo na kuongeza. pato la taifa.

“Tunashirikiana na Serikali katika upandaji miti ili kuokoa maeneo yaliyoharibika, kuonesha uwekezaji katika maeneo ya viwanda na miaka ya hivi karibuni tumeweza kuongeza kiwango cha uwekezaji wa ndani na usafirishaji zaidi mazao ya misitu kuliko ilivyokuwa awali,”.

Akizungumzia sekta ya ufugaji nyuki Profesa Silayo amesema kuwa wanaendelea kuhamasisha wananchi kujihusisha na ufugaji nyuki,uchakataji wa zao la nyuki, kuboresha mnyororo mzima wa thamani pamoja na usafirishaji katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

“Tumepata masoko makubwa nje ya nchi, sasa ni wajibu wa wadau wetu wa ndani wanaofanya biashara za kimataifa kuyakaribia masoko hayo na kufanya biashara ya kimataifa pamoja na kuwezesha nchi kupata fedha za kigeni,”amesema.

Amesema kuwa ufugaji wa nyuki wanaupa kipaumbele kwani kuna masoko ambayo yameshafanyiwa tathmini za ubora wa zao la nyuki nchini na zinakidhi vigezo vya uuzaji kwenye masoko ya nje ya nchi.

Amesema kuwa kumekuwa na mageuzi makubwa katika uwekezaji hapa nchini hasa ukiangalia viwanda vilivyowekezwa vimeleta teknolojia ambazo hazikuzoeleka hapo kabla.

Amewaasa kuzalisha bidhaa zenye ubora wa viwango vya juu ili wasije kuharibu masoko, lakini wazalishe kwa kiwango kikubwa kwani kwa sasa kiwango ni kidogo

Aidha amewaalika wadau mablimbali kutembelea banda lao ili waweze kupata elimu juu ya uwekezaji kwenye sekta mbalimbali zinazosimamiwa na TFS.