Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
MAMLAKA ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)imesema moja ya mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Samia Suluhu Hassan ni katika kipindi chake cha miaka minne ni uanzishwaji wa Mpango Maalumu wa Ruzuku ya Mbolea katika msimu wa kilimo 2022/2023.
Wenye lengo la kupunguza gharama ya mbolea kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo, kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza upatikanaji wa malighafi za viwanda.
Hayo yamesemwa jijini hapa leo Machi 19,2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita ambapo amesema toka kuanzishwa kwa mpango huo hadi kufikia jana wakulima zaidi milioni 4 wamesajiliwa na tani Milioni 1.39 zimeuzwa.
Laurent ameeleza kuwa kabla ya kuanza utekelezaji wa Mpango wa Ruzuku ya Mbolea katika msimu wa 2021/2022, Sekta ya Kilimo ilikabiliwa na changamoto ya kupanda kwa bei ya mbolea katika soko la ndani kutokana na kupanda kwa bei ya mbolea katika soko la dunia.
“Bei za mbolea nchini zilipanda kutoka wastani wa shilingi 70,000/= kwa mfuko wa kilo 50 hadi kufikia shilingi 140,000 hadi 150,000 kwa mfuko.Hali hii ilichangia kushuka kwa matumizi ya mbolea, tija na uzalishaji,”amesema Laurent.
Aidha ameeleza kuwa Mpango huo maalumu wa ruzuku ya mbolea uliwezesha kupunguza gharama ya mbolea na kufanya wakulima kununua mbolea kwa bei ya shilingi 40,000 hadi 80,000 kwa kutegemea aina ya mbolea na umbali sawa na punguzo la takribani asilimia 50 ya bei.
“Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii, Serikali inatekeleza Mpango wa Ruzuku ya Mbolea kwa kutoa ruzuku kwa wakulima wote na kwa mazao yote nchini,”amesema.
Laurent amefafanua kuwa tofauti na ruzuku zilizopita, katika awamu hii ruzuku ya mbolea inatolewa kupitia Mfumo wa Kidijitali wa Ruzuku ya Pembejeo za Kilimo (Agricultural Inputs Subsidy System) ambao unatumika kusajili wakulima, waingizaji, wazalishaji na mawakala wa mbolea pamoja na kuratibu usambazaji na mauzo.
Amesema matumizi ya mfumo wa kidijitali katika kusambaza mbolea ya ruzuku umeinufaisha Serikali hususani katika kuwezesha kuanzisha kanzidata ya kuaminika ya wakulima, Mawakala wa mbolea,waingizaji na wazalishaji wa mbolea nchini.
Vilevile Mkurugenzi huyo amesema katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, biashara ya mbolea nchini imekua kwa kiasi kikubwa ambapo wafanyabiashara wa mbolea waliopewa leseni wameongezeka kutoka 3,069 mwaka 2020/21 hadi 7,302 Februari, 2025.
Huku upatikanaji wa mbolea ukiongezeka kutoka tani 766,024 mwaka 2020/2021 hadi tani 1,213,729 mwaka 2023/2024,uingizaji wa mbolea ukiongezeka kutoka tani 504,122 mwaka 2020/2021 hadi tani 728,758 mwaka 2023/2024 na uzalishaji wa ndani umeongezeka kutoka tani 42,695 mwaka 2020/2021 hadi tani 158,628 mwaka 2023/2024.
Laurent amesema kutokana na kuboreshwa kwa mazingira ya uwekezaji nchini pamoja na utashi wa kisiasa wa Serikali ya Awamu ya Sita Tanzania imeshuduia kuongezeka kwa viwanda vya kuzalisha mbolea na visaidizi vya mbolea kutoka viwanda 16 mwaka 2020/2021 hadi viwanda 33 mwaka 2023/2024. Kati ya viwanda hivyo, vitatu ni vikubwa, viwanda 11 ni vya kati na viwanda 19 ni vidogo.
Pia amesema kumekuwa na ongezeko la matumizi ya mbolea kutoka tani 363,599 mwaka 2020/2021 hadi tani 840,714 mwaka 2023/2024.
“Ongezeko hilo limewezesha kuongezeka kwa matumizi ya mbolea kutoka kilo 19 za virutubisho kwa hekta mwaka 2020/2021 hadi kilo 24 za virutubisho kwa hekta mwaka 2024/2025.
“Lengo ni kufikia kilo 50 za virutubisho kwa hekta ifikapo mwaka 2033 kwa kuzingatia makubaliano ya Wakuu wa Nchi za Afrika yaliyofanyika Nairobi 2024,”amesema.
Laurent amesema kuongezeka kwa matumizi ya mbolea nchini kumechangia kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya chakula kutoka tani 19,980,718 mwaka 2020/2021 hadi tani 22,803,316 mwaka 2023/2024 sawa na ongezeko la asilimia 14 na kufanya utoshelevu wa chakula nchini kufikia asilimia 128.
Pamoja na hayo Mkurugenzi huyo amesema kuwa kwa mara ya kwanza imeandaa Mkakati wa Taifa wa Mbolea na Afya ya Udongo (2024 – 2030) ambao tayari umeanza kutumika.
“Mkakati huu unaweka malengo na mbinu za kuhakikisha upatikanaji, ufikiaji na matumizi ya mbolea kwa wakulima pamoja na ustahimilivu wa tasnia ya mbolea nchini,”amesema.


More Stories
Kamati ya Kudumu ya Bunge Nishati, Madini yaridhishwa na utekelezaji mradi wa TAZA
Serikali yavuna Shilingi Bilioni 3 ndani ya miezi nane
Puma Energy yawataka wakazi wa Dodoma kuchagua nishati safi