Na Mwandishi Wetu
KUTOKANA na kasi ya kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Corona (Covid-19) hapa nchini na Duniani kwa ujumla, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limetangaza utaratibu mpya ili kuwakinga wadau wa soka na maambukizi ya ugonjwa huo.
Hadi jana jioni Shirikisho la Afya Duniani (WHO) lilikuwa limeripoti jumla ya kesi 961,343 vifo vikiwa 49,160 na waliopona ni 203,153 huku kwa hapa nchini Serikali ikithibitisha kuwepo kwa visa 20 vya waliokutwa na ugonjwa huo, kifo kimoja huku wagonjwa wawili wakiruhusiwa kurudi nyumbani.
Kwa mujibu wa Afisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Cliford Ndimbo amesema kuwa, kuanzia jana Aprili 2 watawasiliana na wadau wao kwa njia za barua pepe ikiwa ni njia mojawapo ya kuwakinga na maambukizi hayo hadi pale utaratibu mwingine utakapotangazwa.
Alisema, Sekretarieti imeamua hivyo lakini wataruhusiwa tu kufika katika ofisi za Shirikisho hilo endapo kutakuwa na jambo la muhimu sana litakalowalazimu kuhudumiwa katika ofisi hizo.
“Maamuzi haya yamefikiwa na Sekretarieti ya TFF ikiwa ni moja na jitihada za kuzuia kuendelea zaidi kwa maambukizi ya ugonjwa huu ambao kwa sasa unaitikisa Dunia, kwa wale wadau ambao wana mambo ya kawaida basi wawasiliane na wahusika kupitia namba za simu na barua pepe tulizotoa lakini pia kwa wale watakaokuwa na ulazima sana wa kufika ofini kwetu basi tutawahudumia,” alisema Ndimbo.
Katika hatua nyingine TFF, imewatoa hofu wadau wa soka hapa nchini baada ya kusema kuwa, kumalizika kwa msimu huu wa Ligi kutategemea maamuzi yatakayofanywa na vyombo vinavyosimamia na kuendesha Ligi na Kamati ya Utendaji ya TFF.
TFF walitoa ufafanuzi huo kutokana na taarifa ya mkanganyiko iliyoripotiwa awali lakini ikiwa pia kama ufafanuzi kwa baadhi ya wadau wa soka ambao wameonesha wasiwasi wao wa msimu huu wa Ligi kumalizika kwa wakati.
Kauli iliyotolewa na Mtendaji Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao ilisema kuwa, kama janga la Covid 19 litaendelea, msimu huu utategemea maamuzi yatakayofanywa na vyombo vinavyosimamia na kuendesha Ligi Kuu kwa pamoja na Kamati ya Utendaji ya TFF.
Alisema kuwa, kwa sasa bado ni mapema sana kusema msimu huu umefutwa au kuusogeza mbele hadi Juni 31 kutoka Mei 31.
“Kama janga la ugonjwa huu wa Covid-19 litaendelea basi msimu wa Ligi utategemea maamuzi yatakayofanywa na vyombo vinavyosimamia na kuendesha Ligi Kuu kwa pamoja na Kamati ya Utendaji ya TFF kwani kwa sasa ni mapema sana kusema tumefuta msimu pamoja na kwanza unaweza kwenda mpaka June 31, ” alisema Kidao.
More Stories
15 wajinoa Juventus,akiwemo mtoto wa Mwenyekiti wa CCM Mbeya
Za Kwetu Fashion Show, yawapaisha wanamitindo nchini
TCAA yaadhimisha siku ya usafiri wa anga Duniani kwa kushiriki mbio za Marathon UDSM