January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TET yafuatilia mpango wa mtoto kuanza shule

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online

TAASISI ya Elimu Tanzania (TET) kupitia Programu ya Shule Bora, Desemba 19, 2022 imeanza kufanya ufuatiliaji katika vituo mbalimbali vya Mpango wa Utayari wa kumuandaa Mtoto kuanza Shule katika Mkoa wa Pwani.

Vituo hivyo vya utayari vilianza mwezi Oktoba mwanzoni mwaka huu ambapo watoto watahudhuria kwa wiki kumi na mbili hadi mwishoni mwa mwezi huu kabla ya kuanza darasa la kwanza mwaka 2023.

Akizungumza katika Wilaya ya Bagamoyo kwenye vituo vya Utayari vya Kudibahi na Mikoroshini, Mkurugenzi wa Mafunzo ya Mitaala, Dkt. Fika Mwakabungu amesema kuwa ameridhishwa na namna vituo hivyo vinavyoendesha madarasa hayo ya utayari na kuwa watoto walioweza kuhudhuria wamejifunza na kuwa tayari kuanza darasa la kwanza.

“Kwa kweli kazi kubwa imefanyika kwani watoto wanaonekana kabisa kuelewa kile walichofundishwa na hii imewajengea kujiamini na kuonesha sasa wako tayari kuanza masomo yao ya msingi na kuwa kama watoto wengine walioweza kupitia madarasa ya awali” amesema Dkt. Mwakabungu.

Dkt.Mwakabungu amewapongeza Walimu Wasaidizi wa Jamii wote waliokubali jukumu la kuwaandaa watoto hao katika vituo vyote vya mkoa wa Pwani pamoja na wazazi wote walioweza kuruhusu watoto wao kuandaliwa katika vituo hivyo na amesema kuwa anaamini mwakani watoto wengi wataweza kuletwa katika vituo mbalimbali vya utayari.

Kwa upande wake mwakilishi wa walimu wa vituo hivyo Bi.Neema Taigo amesema kuwa wanafunzi wameonesha uelewa mkubwa katika madarasa hayo na kuwa katika mwaka ujao watoto wengi wataweza kujitokeza kwa wingi.

Naye mwakilishi wa wazazi Bwana. Richard Kwiyela ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuhakikisha Elimu inapatikana kuanzia ngazi ya chini na kwamba, wakazi katika eneo lao watashirikiana na serikali katika kuhakikisha wanajenga shule kuanzia elimu ya Awali hadi Msingi ili kuhakikisha watoto wote wanapata elimu kama wengine.

Mbali na Wilaya ya Bagamoyo, leo pia katika wilaya ya Kibaha DC na Rufiji vituo vya utayari vya Ruvu Dosa, Mnazi, Nyabhanje na Ngomboroni viliweza kutembelewa na kuonekana maendeleo yake na utekelezaji ulivyofanyika wa Mpango wa Utayari.

Mpango huo wa vituo vya Utayari unataekelezwa na Ofisi ya Rais -TAMISEMI kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania(TET) chini ya mradi wa Shule Bora .