January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Teknolojia chanzo Butimba,yaivutia Kamati Baraza la Wawakilishi

Na Judith Ferdinand,Timesmajira Online, Mwanza

Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati, Baraza la Wawakilishi Zanzibar, wamevutiwa na kujifunza teknolojia ya kisasa,inavyofanya kazi kwa ufanisi wa kuzalisha na kusambaza maji, kwa wananchi katika mradi wa chanzo kipya cha maji Butimba,kilichopo jijini Mwanza.

Hayo yamebainishwa Oktoba 7,2024, na Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano,Ardhi na Nishati, Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Yahya Rashid Abdulla,wakati akizungumza na waandishi wa habari,katika ziara ya kutembelea chanzo hicho cha maji Butimba.

Abdulla, ameeleza kuwa lengo la ziara hiyo ni kubadilishana uzoefu katika usimamizi wa maji.Huku akieleza umuhimu wa kujifunza kutoka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) kuhusu mbinu bora za uzalishaji na usambazaji wa maji.

Ambapo ameeleza kuwa,wamejifunza jinsi MWAUWASA, wanavyotumia Ziwa Victoria kuzalisha maji,kisha kuyatibu na kuyasambaza kwa wananchi katika maeneo mbalimbali kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

“Tumejifunza kuwa kuna haja ya watendaji wetu, kuhakikisha wanatumia teknolojia zaidi katika kuwahudumia wananchi ili kuleta ufanisi zaidi,kupata elimu na kubuni vitu vyenye kuleta ufanisi zaidi,”amesema Abdulla.

Pia wamejifunza jinsi MWAUWASA wanavyoyahifadhi na kuyalinda maeneo hayo ya vyanzo vya maji kwa kuwa na hati miliki.

Waziri wa Maji,Nishati na Madini Zanzibar,Shaibu Hassan Kaduara, amesema,lengo ni kubadilishana uzoefu,kuona baadhi ya changamoto ambazo zinawakabili wao Zanzibar,MWAUWASA wanazitatuaje,kwani wanapata maji kutoka chini ya ardhi huku Mwanza yanaonekana.

“Uendeshaji wa maji ni gharama, tumekuja kuangalia wenzetu kwenye maji haya ya Ziwa Victoria wanayatibu vipi,mpaka kufika kwa walaji.Ili maono yetu mbadala kwenda kuangalia uvunaji wa maji ya mvua,na kuweza kuyatibu ili yaweze kwenda kwa walaji,”amesema Shaibu na kuongeza:

“Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,kama ilivyo sera ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) na dira ya maendeleo,ni kuwapatia wananchi wa mjini na ,vijijini maji safi na salama.Jambo hilo tunalisimamia kwa nguvu zote ili wananchi waweze kupata malengo yaliokusudiwa na Serikali,”.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa MWAUWASA,Neli Msuya,amesema chanzo hicho cha maji Butimba kinatoa maji kiasi cha lita milioni 48 kwa siku.Ambapo hali ya upatikanaji maji umeimarika na kufikia asilimia 89,kazi inayoendelea ni kuboresha mifumo ya usambazaji maji.

“Mwishoni mwa wiki iliopita tulipokea mabomba yenye urefu wa kilomita 8, kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji katika maeneo ya Mwanza na tunayoyahudumia,lengo ni haraka iwezekanavyo tuendelee kulilaza,tunakwenda kwenye maeneo ambayo yanapata huduma lakini mabomba yake yamechakaa,ili tudhibiti upotevu wa maji na yaweze kupatikana kwa wananchi kwa urahisi,”.

Pia ameeleza kuwa,mradi huo wa chanzo cha maji,wanashirikina Bonde la Ziwa Victoria kulinda vyanzo vya maji.Pia wameshirikiana na Wakala wa Misitu Tanzania(TFS) ambapo wameanzisha kitalu chenye miti 45,000 katika eneo hilo la mradi.

“Tunashirikiana Gereza na Butimba, wananchi wanaozunguka chanzo hiki cha maji Butimba,kuweza kupanda miti,lengo ni kuhakikisha eneo hili tunalilinda,pia eneo la mita 60,kwenda ziwani linalindwa,”.