December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TEF yapongeza Mkutano Mkuu CCM kuwa LIVE, yashauri maeneo mengine

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, DSM

KUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF), limepongeza uamuzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuruhusu kurushwa moja kwa moja (live) kwenye vyombo vya habari, mikutano yake miwili; Mkutano wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM na Mkutano Mkuu Maalum wa CCM wa 2020.

Taarifa kwa vyombo vya hanati lililotolewa na TEF na kusainiwa na Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa, Deodatus Balile, ilieleza kwamba;

“Tumefarijika zaidi kwa waandishi wa habari kuruhusiwa kuwamo ndani ya ukumbi wa Mkutano tangu mwanzo wa mkutano hadi ulipofungwa. Kadhalika tumevutiwa na utaratibu mpya na wa aina yake, ambao umewezesha kura za wagombea urais ndani ya CCM kwa Zanzibar na Muungano kuhesabiwa ‘live’ huku vyombo vya habari vikishuhudia.

Hii ni hatua inayoongeza uwazi na kuziba mianya ya malalamiko. Hakuna anayeweza kulalamika au kuwa na mashaka kuhusu kura za mgombea Urais wa Zanzibar, kwani wafuatiliaji wa matangazo ya moja kwa moja walioko ndani na nje ya nchi, walishuhudia jinsi washindani walivyokuwa wakikabidhiwa kura zao kadri zilivyokuwa zinahesabiwa,” ilieleza taarifa hiyo ya TEF na kuongeza;

“Hatua hii imeondoa uwezekano wa kutiliwa shaka uteuzi wa mgombea urais wa CCM Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi. Sisi TEF tunaamini utaratibu huu umefuta mianya ya mtu/watu kulalamika kuwa huenda kura zake/zao ‘zilichezewa’.

Vivyo hivyo kwa kura za mgombea urais wa Muungano kupitia CCM, zamu hii ilipotangazwa kuwa amepata asilimia 100, pia hakukuwa na mashaka kwani vyombo vya habari vilishiriki hatua zote kuwahabarisha wananchi mchakato huo wa uteuzi.”

Taarifa hiyo imefafanua kwamba kila aliyefuatilia mikutano hiyo anakuwa kwenye nafasi ya kukiri uhalisia wa mambo yalivyokuwa na kuondoa dhana iliyokuwapo awali kuhusu kile kilichowahi kubatizwa jina la kura za ‘itifaki’ Ni ushauri wetu kwamba utaratibu huu wa CCM ambacho ni chama tawala, uhamie kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Tume Huru ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Mahakamani na Bungeni, kwani mambo wanayojadili ni kwa maslahi ya taifa letu wa watu wake.

Taarifa hiyo ilieleza kwamba vyombo vya habari vikiwa mshirika mkubwa katika kuimarisha amani, usalama na kukuza uchumi kwa kusukuma maendeleo ya nchi, vinatekeleza wajibu wake huo vyema zaidi pale vinapopata fursa za kuripoti uhalisi wa mambo.