August 11, 2022

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TEA kutumia Sh. Bilioni 8.9 kufadhili miradi ya kuboresha miundombinu ya elimu nchini

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 Mamlaka ya Elimu Tanzania imepanga kutumia kiasi cha Sh. Bilioni 8.9 kwa ajili ya kufadhili miradi ya kuboresha miundombinu ya elimu nchini.

Hayo ameyasema jana (Agosti 4, 2022) Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu Tanzania, TEA, Bahati Geuzye wakati akizungumza na waandishi wa habari akitoa ufafanuzi wa Bajeti ya TEA kwa mwaka wa fedha 2022/23 na kusema kuwa Miradi itakayofadhiliwa ni pamoja na Ujenzi wa madarasa 99, matundu ya vyoo 792, maabara kumi za masomo ya sayansi kwa ajili ya shule 05 za sekondari, nyumba za walimu 52 na Mabweni 10.

“Kiasi hicho cha fedha kitatumika kufadhili wa miradi 96 katika shule 96 za msingi na sekondari katika maeneo mbali mbali ya Tanzania Bara pamoja na Taasisi mbili za elimu ya juu kwa upande wa Tanzania Zanzibar.”

Geuzye alisema Miradi mingine itakayotekelezwa ni ujenzi wa miundombinu ya wanafunzi wenye mahitaji maalum inayojumuisha madarasa 10, matundu ya vyoo 40 pamoja na mabweni mawili katika shule 6 za msingi na moja ya sekondari.

Aidha Geuzye alisema Kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa unaoratibiwa na TEA, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Sh. Bilioni 8.6 ziligharimia ufadhili wa miradi 160 ya kuboresha miundombinu ya elimu katika shule 151.

“Miradi hiyo ilijumuisha ujenzi wa madarasa 210 katika shule 65 (za msingi 53 na sekondari 22), Maabara 4 za sayansi katika Shule 2 za Sekondari, Matundu ya vyoo 1920 katika shule 80 (za msingi 58 na sekondari 22), vifaa vya kujifunzia na kufundishia katika shule 09 za wanafunzi wenye mahitaji maalum(shule 08 za msingi na moja ya sekondari) na ujenzi wa ofisi mbili za walimu katika shule mbili za sekondari.”

Mbali na hayo Geuzye alisema TEA ilipokea michango na kutekeleza miradi ya pamoja na mashirika ya Umma na yasiyo ya kiserikali yenye thamani ya Sh. 556.3 mashirika hayo ni pamoja na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Taasisi ya Flaviana Matata, BRAC- Maendeleo Tanzania, Taasisi ya Asilia Giving, Taasisi ya SAMAKIBA na Kampuni ya Dash Industries.

Pia Geuzye alisema Kupitia mfuko wa Kuendeleza ujuzi kiasi cha Sh. Milioni 385.8 imetolewa kunufaisha vijana 1,018 katika programu ya Utarajari (Internship Program) katika sekta za TEHAMA, Utalii na huduma za ukarimu; Nishati; Ujenzi na Uchukuzi.

Geuzye alisema Mfuko wa SDF pia unafadhili mafunzo ya Ujuzi kwa wanufaika 4,000 kutoka Kaya Maskini na Makundi Maalum (Bursary Scheme) hadi ifikapo Desemba 2022 lengo ni kuwezesha vijana wanaotoka katika kaya maskini kupata ujuzi na kujikwamua kiuchumi.

katika kuunga mkono azma ya Serikali ya kuhamia Makao Makuu ya nchi Jijini Dodoma na kutokana na ongezeko la watumishi wa umma na wananchi kuhamia Dodoma, TEA iliona kuna umuhimu wa kuboresha na kukarabati baadhi ya shule za msingi ili kukabiliana na ongezeko la wanafunzi katika Mji huo.

“Mradi huo ulilenga kukarabati na kupanua miundombinu ya shule 4 za msingi za Kizota, Medeli, Kisasa na Mlimwa C. Kiasi cha Sh. Bilioni 1.9 zilitumika. Aidha, TEA inafadhili ujenzi wa Shule ya Msingi ya Mchepuo wa Lugha ya Kiingereza katika Jiji la Dodoma wenye thamani ya Sh. Milioni 750, mradi ambao unasimamiwa na Halmashauri ya jiji la Dodoma. Pia Mfuko wa Elimu umefadhili ujenzi wa Jengo la Hanga kwa ajili ya mafunzo ya Uandisi wa Matengenezo ya Ndege katika Chuo cha Karume cha Sayansi na Teknolojia kilichopo Zanzibar.”

Tangu kuanzishwa kwake, Mamlaka imewezesha utekelezaji wa miradi 3,314 yenye thamani ya Sh. Bilioni 212.6 ambapo taasisi za elimu zikiwemo shule za awali, shule za msingi, shule za sekondari, vyuo vya ualimu, vyuo vya ufundi na vyuo vikuu vimenufaika.