May 21, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TDB yaonya wanaonunua maziwa kwenye chupa za plastiki

Na Mwandishi wetu,TimesmajiraOnline,Dar

BODI ya Maziwa Tanzania(TDB)imeitaka jamii kuacha kununua maziwa ya Ngo’mbe holela yanayouzwa kwenye chupa za plastiki na badala yake watumie maziwa salama na yaliosindikwa kwa afya bora.

Rai hiyo imetolewa Jijini Dar es salaam mapema leo Mei 20, 2025 Mwakilishi wa Msajili wa bodi ya Maziwa Deorinidei Mng’ong’o wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uelewa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali kuelekea Kilele cha wiki ya kitaifa ya Maziwa inayotarajia  kufanyika Mei, 27 hadi Juni Mosi mwaka huu Mkoani Morogoro.

Amesema maziwa ya Ngo’mbe yanayouzwa mtaani kwenye chupa usalama wake ni mdogo mno  kutokana kuwekwa katika mazingira yasiyo salama kwa afya ya  mlaji.

“Chupa ya Plastiki sio kifugashio maalumu kwa ajili ya Maziwa tunajiweka katika hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza kutokana na kutumia maziwa kiholela”amesema

Pia ameongeza kuwa bodi hiyo imekuwa ikifanya uhamasishaji wa unywaji wa maziwa salama na yaliosindikwa kwa afya bora.

Amesisitiza kuwa maziwa ni chakula chenye virutubisho na kueleza kuwa yanapowekwa katika mazingira yasiyo salama ufuatwa na vijidudu jambo  ambalo ni hatari kwa mlaji na mfanyabiashara pia.

Amesema kuwa bodi hiyo imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali ikiwemo kutoa elimu na kuamasisha wafugaji kupata mbegu bora.

Aidha aliwaomba waandishi wa habari kupeleka elimu sahihi kwa jamii  waliyoipata juu ya matumizi ya Maziwa salama.

Kwa upande wake Ofisa Jinsia Lishe, Ruth Mkope amesema maziwa ya Ngo’mbe yanavirutubisho vya aina nyingi  hivyo huweza kuwa mlo kamili kwa watu wote.

“Unywaji wa maziwa inapaswa kupewa msukumo kwa watoto wa Shule wenyewe bila kutegemea wafadhili”amesema

Amesema kwa upande wa mtoto maziwa ni chanzo cha virutubisho vingi vinavyohitajika kwa ajili ya ukuaji na maendeleo ya mtoto.

“Maziwa usaidia kuimarisha kinga ya mwili ya mtoto lakini maziwa ya wanyama hayatumiki kwa watoto chini ya mwaka mmoja “alisisitiza Mkope

Aidha amesema Shirika la Afya linashauri unywaji wa lita 200 kwa mtu mmoja kwa mwaka  sawa na mililita 500 kwa mtu mmoja kwa siku.