March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TCU yasitisha udahili wanafunzi wa shadaha ya udaktari wa binadamu mwaka wa kwanza  chuo cha MzU

Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza

TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imesitisha  udahili na usajili wa wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Shahada ya Udaktari wa Binadamu  Chuo Kikuu Mwanza (MzU) kwa mwaka wa masomo 2025/2026.

Hiyo ni baada ya Tume hiyo kubaini ukiukwaji wa taratibu za udahili  na usajili wa wanafunzi wa shahada ya kwanza  katika chuo hicho Cha MzU uliovuka viwango vilivyoidhinishwa.

Akizungumza na waandishi wa habari Desemba 2,2025, jijini Mwanza Katibu Mtendaji wa TCU, Prof. Charles Kihampa, amesema hatua hiyo imechukuliwa baada ya kubainika kuwa chuo hicho kimedahili idadi ya wanafunzi mara kumi zaidi ya kiwango kilichoidhinishwa na mamlaka ya urekebu(TCU), kwa shahada ya udaktari wa binadamu.

“Idadi husika ni kubwa kuliko uwezo wa chuo kimiundombinu ya kujifunzia na kufundishia ikiwemo idadi ya walimu waliopo,”amesema Prof.Kihampa.

Amesema kuanzia Julai 15 hadi Oktoba 20, mwaka huu TCU iliratibu maombi ya udahili kwa wanafunzi wa Shahada ya kwanza kwa mwaka wa masomo 2025/26 katika vyuo vyote nchini.

Ambapo maombi hayo ya udahili yalitumwa moja kwa moja vyuoni, na vyuo hivyo kuendelea na utaratibu wa udahili kupitia Seneti zao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za udahili na uendeshaji wa elimu ya chuo kikuu nchini.

Amesema,baada ya kukamilika kwa udahili, TCU ilifanya ukaguzi wa awali ili kuthibitisha uzingatiaji wa vigezo mbalimbali, ikiwemo idadi ya wanafunzi kwa kila programu, sifa za kitaaluma na vigezo vingine  stahiki  vilivyoidhinishwa na  Tume hiyo pamoja na bodi au mabaraza ya usajili wa wataalamu.

Prof. Kihampa,amesema  chuo hicho kimedahili na kusajili idadi kubwa kuliko ilivyoidhinishwa katika programu ya Udaktari wa Binadamu kwa mwaka wa masomo 2025/2026. 

Pia amesema,time hiyo katika kikao chake maalum cha 127, kilichofanyika Novemba 28,2025,imefanya maamuzi ya kusitisha kibali cha udahili na usajili wa wananfunzi wa mwaka wa kwanza  wa shahada ya udaktari kwa mwaka wa masomo 2025/2026 wa chuo hicho.

“Chuo Kikuu Cha Mwanza kilizhindwa kufanya marekebisho ya idadi hiyo licha ya kupewa maelekezo ya kufanya  hivyo.Chuo hicho kitaendelea  kutoa mafunzo  kwa wanafunzi wengine wanaondelea na masomo,”amesema Prof. Kihampa na kuongeza:

“Pia imetoka kibali kwa kuwapa fursa wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliodahiliwa,kusajiliqa na kuripoti chuoni  hapo,kuomba  kuhamia kwenye vyuo vingine vilivyoruhusiwa kudahili wanafunzi katika programu ya udaktari wa binadamu au programu nyingine wanazozitaka kwa mwaka wa masomo 2025/26 au miaka inayofuata,”.

Sanjari na hayo  MzU kimetakiwa kuwajulisha wanafunzi kuhusu hatua hiyo na kuwasaidia  katika mchakato wa uhamisho na kuhakikisha wanaelekezwa kwenye vyuo vyenye uwezo na vibali halali vya kuwapokea.

TCU imewahakikishia wanafunzi kuwa mchakato huo utafanyika kwa haraka na kwa kuzingatia maslahi ya wanafunzi na jamii.

Kadhalika amesema, tume hiyo  imeunda kamati maalum ya wataalamu itakayochunguza kwa kina mchakato wa masuala ya kitaaluma katika chuo cha MzU,ambayo itaanza kazi mara baada ya kukamilika kwa mchakato wa uhamisho.

 Hata hivyo amesisitiza kuwa tume hiyo itaendelea kusimamia ubora wa elimu ya juu nchini, kuhakikisha vyuo vyote vinazingatia sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa elimu ya chuo kikuu.

Aidha, Tume imeahidi kuchukua hatua stahiki kila inapobainika uvunjifu wa taratibu ili kulinda viwango vya elimu kitaifa na kimataifa.