November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Katibu Tawala wa Manispaa ya Morogoro, Ruth John, (kushoto), akimkabidhi kitambulisho cha ujasiliamali, mfanyabiashara ndogo ndogo wa Manispaa ya Morogoro, Matha Andason katika halfa ya kukabidhi vitambulisho 99 vya ujasiliamali ambavyo shirika la TCRS limewalipia wafanyabiashara hao. Na Mpigapicha wetu.

TCRS yatoa vitambulisho 99 vya Wajasiriamali Morogoro

Na Penina Malundo, timesmajira Online

SHIRIKA la Kikristu la kuwahudumia wakimbizi la Tanganyika (TCRS), limetoa msaada wa kuwanunulia vitambulisho 99 wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama machinga katika Manispaa ya Morogoro.

Afisa Mwezeshaji wa Shirika hilo, Gasper Werema, amesema shirika la TCRS limekuwa likifanya kazi na kuwasaidia wafanyabiashara wadogo kwa kuwapa misaada, elimu na mafunzo ya biashara ili waweze kujikwamua.

Amesema, shirika hilo linazingatia kuwa wafanya biashara wadogo wengi wao wana mitaji midogo hivyo ni vema kuwainua.

Werema amesema, baadhi yawafanyabiashara hao ikiwa watatoa 20,000 kugharamia kitambulisho cha ujasiliamali huenda wakayumba kimtaji, hivyo wameona watoe vitambulisho 99 kwa wafanya biashara wadogo wa Manispaa ya Morogoro

“Utoaji wa vitambulisho hivi ni mwendelezo wa shughuli zetu za kuwawezesha wafanya biashara wa Manispaa ya Morogoro ili waweze kufanya biashara kwa uhuru.” amesema Werema.

Naye Ofisa Tawala wa Wilaya ya Morogoro, Ruth John, amesema wafanyabiashara hao pamoja na kuwa na vitambulisho vya ujasilamali wanapswa kufuata sheria za Manispaa.

“ Tunawashukuru wenzetu wa shirika la TCRS kwa kutuunga mkono sisi serikali katika juhudi zetu za dhati za kuhakikisha kuwa tunaendelea kuweka utaratibu mzuri na rafiki kwa wafanya biashara ndogo ndogo ili waweze kufanya biashara zao kwa uhuru na uhakika,” amesema na kuongeza

“Ninawaasa wafanyabiashara ndogo ndogo, kuendelea kufuata sheria za serikali za mitaa na Manispaa ikiwa ni pamoja na kuwa na vitambulisho vya ujasiliamali ambavyo Rais John Pombe Magufuli ameleta mpango huu ili kuwapunguzia ushuru na tozo mbali mbali wafanya biashara ndogo ndogo nchini,” amesema

Ruth ameaema Wilaya ya Morogoro itaendelea kushirikiana na mashirika mbali mbali ikiwemo TCRS ili kuboresha hali za wafanya biashara wadogo wilayani hapa.

Akizungumzia msaada huo mfanyabiashara ndogo ndogo wa mboga mboga na matunda katika soko la Mawenzi Manispaa ya Morogoro, Yusuph Mgoha, amesema msaada huo wa kulipiwa vitambulisho vya ujasiriamali utawaongezea hari ya kufanya biashara wakiwa huru huku wakiondokana na mgongano kati yao na mamlaka za manispaa.