Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Jabir Bakari amesema katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na maendeleo makubwa ya sekta ya mawasiliano duniani na hapa nchini .
Dkt Bakari ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam wakati akifungua semina ya wadau wa sekta ya mawasiliano iliyoandaliwa na TCRA katika kuelekea maadhimisho ya usalama mtandaoni.
Maadhimisho hayo huadhimishwa kila jumanne ya pili ya mwezi Februari kila mwaka ambapo uunganisha mamilioni ya watu wote ulimwenguni kwa kuamasisha matumizi ya mawasiliano sahihi na salama yenye tija.
Dkt.Bakari amesema jamii ya watanzania vijijini na mijini imefikiwa na huduma hiyo ya mawasiliano ambapo taarifa ya mwisho ya robo ya mwaka inayoishia Desemba 2023 imeonesha idadi ya watumiaji wa intaneti katika nchini hapa imefikia takribani milioni 35.8 huku idadi ya simu janja ambazo zinauwezo wa kutumia intaneti nazo zimefika milioni 19.8.
“Takwimu hizi zinaonesha ukuaji mkubwa wa matumizi ya intaneti pia utaona katika takwimu laini za simu zimefikia takribani milioni 70,upatikanaji na unafuu wa huduma mbalimbali za mawasiliano nchini ni uthibitisho kuwa serikali imejipanga vyema kuandaa mazingira bora na wezeshi kwa watanzania pamoja na kuwaanda ipasavyo katika uchumi kidigiti”amesema.
Aidha amesema mazingira hayo yanaboresha utoaji wa huduma za jamii pamoja na kuwafikia Watanzania wengi mjini na vijijini,kuzalisha ajira, kuongeza pato la taifa, kufungua fursa mpya kwa ajili ya maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii katika nchi na kuboresha maisha ya kila Mtanzania.
Vilevile amesema katika dhama za maendeleo ya teknolojia ya kidigiti kila mmoja ana nafasi muhimu kuhakikisha anga la mtandao ni salama kwa kuzingatia matumizi sahihi na salama yanayoleta tija kwa mtu binafsi, jamii na Taifa hivyo elimu ya matumizi ya teknolojia za kidigiti ni muhimu sana.
“Pamoja na faida nyingi zitokanazo na tehama bado tunawajibu wa kuendelea kuelimishana kwani kuna baadhi ya watumiaji wamekuwa wakitumia fursa hiyo pamoja na fursa nyingine kufanya uhalifu hivyo tunawajibu wa kuwadhibiti na kuwapatia elimu, “amesema Dkt. Bakari.
Akizungumzia maadhimisho hayo Dkt.Bakari amesema ni mpango wa kimataifa ulioanzishwa mwaka 2004 Kwa lengo la kuhamasisha matumizi sahihi na salama ya mtandao intaneti.
” Semina hii ni kielelezo tosha cha hatua zinazochukuliwa na TCRA katika kuhakikisha elimu ya matumizi sahihi salama ya mtandao pamoja na kuwafikia wadau wote wa sekta ya mawasiliano ndio rasilimali muhimu katika kujenga uchumi wa kidigiti ambao ukuaji wake unategemea sana matumizi chanya ya teknolojia,”amesisitiza.
Naye mmoja wa washiriki katika semina hiyo, Dkt. Macca Abdalla amesema mtandao umemrahisishia matumizi mbalimbali ya teknolojia.
Aidha amesema bado ipo haja ya baadhi ya wanawake wanahitaji kupata elimu zaidi ya mtandao ili waweze kujikwamua kiuchumi.
More Stories
Wanafunzi 170 wapata ufadhili wa masomo
Maelfu kunufaika namsaada wa kisheria Katavi
Serikali yazidi kuwakosha wawekezaji wadau waipa tano