Na Mwandishi wetu,Timesmajira
KUPITIA Mpango wa Mafunzo ya Ufundi kwa Sekta ya Madini (IMTT) unaoendeshwa na Chemba ya Migodi Tanzania (TCM) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufunzi Stadi (VETA), umesaidia vijana zaidi ya 1,500 kupata ujuzi unaowawezesha kufanya kazi katika migodi na kwenye viwanda mbalimbali nchini.
Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam jana tarehe i 23/5/2025 na Katibu Mtendaji wa TCM, Benjamin Mchwampaka wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema kati ya vijana hao waliopata ujuzi huo 1,333 ni wanaume na wanawake ni 167 na kwamba asilimia 70 ya wahitimu hao wote wamepata ajira migodini na viwandani ndani na nje ya nchi.
Amesema mpango huo wa mafunzo ambao ulianzishwa mwaka 2009 ulilenga kukabiliana na uhaba wa mafundi mchundo waliobobea katika sekta ya madini hali iliyosababisha migodi kuajiri watalaamu kutoka nje ya nchi kama Ghana, Mali na Afrika Kusini na kwamba kwa sasa utegemezi wa wataalamu hao kutoka nje umepungua na kusaidia fedha za mishahara kubaki nchini.
“Kupitia IMTT zaidi ya vijana 1,500 wa kitanzania wamehitimu katika maeneo matano ya msingi ambayo ni ufundi umeme wa viwandani, ufundi wa mitambo mikubwa ya migodini, umeme wa magari migodini, uungaji vyuma vizito na ufundi wa mitambo na ufitishaji,” amesema

Mchwampaka na kuongeza“Hata hivyo kwa sasa ambapo migodi mingi imehamia kwenye uchimbaji wa chini ya ardhi, mahitaji ya kitaalamu yameongezeka, TCM na Veta tumeanfdaa kozi mpya sita ambazo zipo katika hatua za mwisho kuidhinishwa, kozi hizo ni uendeshaji wa mitambo ya jumbo na solo, uendeshaji wa Bogger na Cubex, utengenezaji na kuchaji baruti mashimoni pamoja na kuinua lifting na rigging,” amesema.
Amesema kozi hizo zitaandaa vijana wa kitanzania kuchukua nafasi zinazoshikiliwa na wataalamu kutoka nje na kusaidia kutekeleza sera ya ushiriki wa watanzania katika sekta ya madini.
“TCM inaunga mkono juhudi za serikali za kuongeza ushiriki wa Watanzania kwenye mnyororo wa thamani kwa kuwaandaa wahitimu kwa ujuzi unaohitajika sokoni ili kupanua fursa za ajira na kuchangia katika maendeleo jumuishi ya uchumi wa taifa, tunashauri jamii kuchangamkia fursa,” amesema
Hata hivyo amesema vijana wote wa kitanzania wenye elimu kuanzia kidato cha nne wanakaribishwa kujiunga kusoma kozi hizo ambazo zitawafanya kupata fursa ya kufanyakazi migodini.
More Stories
Airtel Tanzania yaungana na Infinix kuzindua NOTE 50 Pro+
Jiji la Dar-es-Salaam latenga bilioni 18 za mkopo wa asilimia 10
Yas yatoa msaada wa vifaa Hospitali ya Bombo Tanga