May 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TCD yazindua majukwaa ya majadiliano ngazi ya wilaya katika wilaya mbili

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Mwanza

Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kimezindua majukwaa ya majadiliano katika wilaya mbili za Nyamagana (Mwanza) na Kasulu (Kigoma) ambayo yataviwezesha vyama vya siasa kujadili tofauti zao.

Lengo la kuundwa kwa majukwaa hayo ni kukuza, kuimarisha na kudumisha demokrasia ya siasa ya vyama vingi hapa nchini na mradi huo wa kuunda majukwaa ya majadiliano umefadhiliwa na Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania.

Katika uzinduzi huo uliofanyika leo Julai 21, 2023 katika wilaya hizo, wajumbe kutoka vyama mbalimbali vya siasa nchini wamewachagua viongozi wao ambapo Nyamagana wamemchagua Salum Mkumbukwa (Cuf) kuwa mwenyekiti na Geoffrey Kavenga (CCM) kuwa katibu wa TCD wa wilaya hiyo.

Vilevile, TCD imezindua majadiliano ya vijana kutoka vyama vya Siasa kuhusu Sheria ya Vyama vya Siasa, Sheria ya Taifa ya Uchaguzi na mzunguko wa uchaguzi koani Dodoma.

Mjumbe wa TCD Taifa, Victory Mnyaga amesema jukwaa hilo litatumika kubainisha changamoto za kisiasa zinazoibuka na kuzijadili kisha kuzitafutia mwarobaini wake.

“Jukwaa hili litafanya vikao na kujadili changamoto za kisiasa na kutafuta mwafaka wake. Kama kuna migogoro baina ya vyama vya siasa ambayo inaweza kutatuliwa katika ngazi hii itapatiwa ufumbuzi,” amesema Mnyaga.

Mwenyekiti wa TCD wilaya ya Nyamagana, Salum Mkumbukwa ameishukuru TCD kwa hatua hiyo huku akiahidi kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa kanuni zinazoongoza jukwaa hilo.

“Tumekuwa tukipitia changamoto na migogoro mbalimbali ya kisiasa katika maeneo yetu. Pamoja na kwamba bado Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaendelea na maridhiano lakini jukwaa hili litatusaidia kuwa sehemu ya kutatua changamoto zetu,” amesema Mkumbukwa.

Kikao cha jukwaa hilo kimehudhuriwa na watu zaidi ya 25 wakijumuisha wenyeviti, makatibu na wajumbe wa kamati tendaji za vyama vya siasa ikiwemo CCM, Chadema, CUF, ACT Wazalendo na mwakilishi kutoka Asasi za Kiraia (Azaki).