Na Judith Ferdinand, Mwanza
BODI ya Pamba Tanzania (TCB) imesema katika msimu huu wa kilimo, ugawaji na usambazaji wa pembejeo za pamba hapa nchini utasimamiwa kupitia mfumo wa kidijitali.
Mabadiliko hayo yamebainishwa katika taarifa iliyotolewa Oktoba 30, 2026 na Mkurugenzi Mkuu wa TCB, Mhandisi Godwin Makori, ambapo imeeleza kuwa lengo la mfumo huo ni kuimarisha uwazi, udhibiti, uwajibikaji, na kuhakikisha pembejeo zinawafikia wakulima wanaostahili kwa wakati.
Mha.Makori amesema,mfumo huo wa utafuatilia pembejeo kuanzia zinapotolewa ghalani hadi zinapomfikia mkulima kupitia hatua nne kuu ambazo ni utoaji wa pembejeo ghalani, uthibitishaji wa mapokezi kwenye Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS), ugawaji kwa mkulima pamoja na uhakiki na uhuishaji wa taarifa.
“Ili kupata pembejeo hizo, anatakiwa kuwa mkulima wa pamba katika msimu husika na awe amesajiliwa kwenye mfumo huo. Mkulima ambaye hajasajiliwa atasajiliwa palepale kituoni, wakati wale waliosajiliwa tayari watatakiwa kuhuisha taarifa zao kama kuna mabadiliko yoyote,”.
Sifa nyingine muhimu ni mkulima kuwa na Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIDA) pamoja na namba ya simu inayofanya kazi kwa ajili ya kupokea ujumbe mfupi wa siri wa uthibitisho (OTP) wakati wa kupokea pembejeo hizo.
Hata hivyo, TCB imesema hakuna mkulima anayestahili atakayekosa pembejeo katika msimu huu kwa sababu tu ya kukosa namba ya NIDA.Huku
bodi hiyo imeeleza kuwa inaendelea kushirikiana na NIDA ili wakulima wasio na namba watambuliwe na kuzipata haraka, huku ikiwahimiza wakulima kujitokeza kuzifuatilia kwa kuwa namba hizo zinahitajika pia katika huduma nyinginezo.
Kupitia utaratibu huo mpya, TCB inalenga kuimarisha udhibiti, kupunguza upotevu na matumizi yasiyokusudiwa ili pembejeo ziwafikie walengwa wenyewe.
Kufuatia hatua hiyo, viongozi wa Serikali za Vijiji na Mitaa,AMCOS, pamoja na wataalamu wa kilimo wameombwa kushirikiana kwa karibu ili kuelimisha wakulima kuhusu utaratibu huo mpya ili wapate pembejeo zao kwa wakati.

More Stories
Dkt. Tulia atoa vifaa kukamilisha ujenzi daraja Itezi
Tanzania yapokea uenyekiti wa Baraza la LTA
Malolo wafurahia maboresho miundombinu ya elimu