December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maofisa wa TBS wakifanya ukaguzi kwenye moja ya maduka ya kuuza vipodozi wilayani Kinondoni, jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Katika ukaguzi huo aina mbalimbali za vipodozi zaidi ya 50 vilivyopigwa marufuku katika siko la Tanzania vilikamatwa.

TBS yakamata vipodozi vilivyopigwa marufuku

Na Mwandishi Wetu

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limekamata aina mbalimbali zaidi ya 50 ya vipodozi vilivyopigwa marufuku kutumika nchini baada ya maofisa wake kufanya ukaguzi wa kushtukiza katika duka la kuuza bidhaa hizo lililopo Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Vipodozi hivyo vilikamatwa mwisho mwa wiki. Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Ofisa Udhibiti Ubora na Mtathmini na Msajili wa Bidhaa za Vipodozi wa TBS, Mboni Mwampeta, alisema katika ukaguzi huo walimkuta muuzaji akiwa anauza bidhaa ambazo hazitakiwi kuwepo sokoni kutokana na kuwa na viambata sumu ambavyo vina madhara kwa watumiaji ikiwemo kusababisha kansa.

Alitoa mfano akisema kwenye ukaguzi wao huo, walikutana na sabuni na losheni aina aina ya Botuoer ambayo haijulikani imetengenezwa na vitu gani ndani yake.

“Lakini pia tumekuta muuzaji akiwa na vipodozi vyenye lugha ambayo haitakiwi kuwepo kwenye soko letu la Afrika Mashariki. Lugha ambazo zinatakiwa kuelezea bidhaa husika kwenye vifungashio ni Kiswali, Kiingereza na Kifaransa, lakini hiyo ina maandishi ya kiarabu,” alisema Mwampeta na kuongeza;

“Pia tumekuta muuzaji anatengeneza mkorogo nchini, akiwa na makopo ambayo yapo tupu , hivyo anachanganya mkorogo na kuweka kwenye makopo ya losheni, akija mteja anadhani losheni hiyo imetoka kiwandani, kumbe imetengenezwa dukani.”

Alitoa wito kwa wauzaji, waagizaji na watengenezaji wa vipodozi kwenda TBS kusajili bidhaa zinazotoka nje ya nchi. Kwa upande wa wazalishaji hapa nchini aliwataka waende TBS kwa ajili ya kupata nembo ya alama ya ubora.

“Lakini pia tunawashauri wauzaji wa maduka wanapoenda kununua kwenye maduka ya jumla wahakikishe muuzaji ana cheti cha usajili wa hiyo bidhaa inayohusika ili kuepukana na hasara kama ambayo mwenzetu ameipata,” alisema Mwampeta na kusisitiza;

“Lakini pia tunawashauri kuiingia kwenye tuvuti ya shirika kwa ajili ya kusajili maeneo yao ya uuzaji wa vipodozi pamoja na chakula.”

Alipouliza hatua zinazoendelea baada ya kukamata vipodozi vilivyopigwa marufuku, Mwampeta alisema kwanza ni kuviteketeza ambayo ni hasara kwa muuzaji, kitu ambacho wao kama shirika hawapendi kitokee na pili wana taratibu za ndani za kisheria ambazo muuzaji atazipata.

Kwa upande wake Ofisa Masoko wa TBS,Mussa Luhombero, alisema ukaguzi huo ni mwendelezo wa kaguzi ambazo zimekuwa zikifanyika sokoni ili kuondoa kwenye soko vipodozi ambavyo tayari vimepigwa marufuku hapa nchini.

Alisema kuna vipodozi vya aina tofauti ambavyo vimepigwa marufuku nchini visitumike, lakini walifanikiwa kuvikamata kupitia ukaguzi huo.

Alitoa wito kwa wauzaji, watumiaji wahakikishe wananunua vipodozi ambavyo vimepigwa marufuku na wenye maduka ya kuuza vipodozi wahakikishe wanasajili bidhaa hizo.