November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TBS Kanda ya Magharibi yafanya ukaguzi wa kushtukiza, usajili

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online Kigoma

SHIRIKA la Viwangi Tanzania (TBS) kwa kushirikishana na mkoa na Halmashauri za Kigoma limeendelea na ukaguzi wa kushtukiza sokoni kwa wasambazaji na wauzaji wa bidhaa za vilainishi, vipuli vya magari, vifaa ya ujenzi, chakula na vipodozi ili kuhakikisha zinakidhi ubora wa kiwango.

Ukaguzi huo uliofanyika Kanda ya Magharibi mkoani Kigoma katika wilaya za Kakonko, Kibondo, Buhigwe, Kasulu, Uvinza na Kigoma ni endelevu.

Ukaguzi huo wa maofisa wa TBS uliofanyika katika maeneo ya uzalishaji na wakati zikiingizwa kutoka nje ya nchi unalenga kupunguza tatizo la uwepo wa bidhaa hafifu sokoni zikiwemo zile zinazoingizwa kupitia njia zisizo rasmi au kuzalishwa kwa kutozingatia matakwa ya kiwango husika.

Mkaguzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Elisha Meshack (aliyeinama mbele) akiwa katika ukaguzi wa bidhaa za ujenzi vinavyouzwa sokoni, wilayani Kasulu, mkoani Kigoma wiki hii, ambapo sampuli huchukuliwa na kupelekwa kwenye maabara za shirika hilo kuzihakiki kama bidhaa zinazosambazwa sokoni zimekidhi ubora wa kiwango husika. Na mpiga picha wetu.

Ukaguzi huo ulienda sambamba na utoaji elimu kwa wauzaji na wanunuaji juu ya uhifadhi sahihi wa bidhaa na umuhimu wa kuzingatia na kusoma taarifa sahihi na muhimu katika vifungashio.

TBS imefanya ukaguzi huu sambamba na usajili wa majengo ya chakula na vipodozi ili kuhakikisha majengo husika yanazingatia ubora na usalama wa bidhaa za chakula na vipodozi vinavyohifadhiwa au vinavyouzwa ndani ya majengo hayo.

Kaimu Mkuu wa Kanda ya Magharibi wa TBS, Rodney Alananga ametoa wito kwa waingizaji na wauzaji wa bidhaa zilizo katika viwango vya lazima kuzingatia sheria na taratibu za uingizaji na uuzaji bidhaa kwa kuuza na kuingiza bidhaa ambazo ni bora na salama ili kukuza biashara na kuepuka kupoteza masoko na kero ya kukutwa na bidhaa hafifu ambayo itawalazimu kuziteketeza kwa gharama zao.

Wakaguzi wa TBS wakiwa katika ukaguzi wa kawaida katika kiwanda cha kuzalisha maji ya kunywa wilayani Kibondo kijulikanacho kama ” Malagarasi Mineral General Supply”. TBS inawahimiza wazalishaji kuthibitisha ubora wa bidhaa zao ili kuepuka usumbufu.

Pia amewashauri wasisite kuwasiliana na ofisi ya TBS mara kwa mara pale wanapohitaji msaada wa kitaalamu.

Kwa upande wake Afisa Usalama wa Chakula TBS, Elisha Meshack amesema ukaguzi huo ni iendelevu, kwani ni moja ya majukumu ya Shirika na utahusisha bidhaa mbalimbali katika sekta zote kasoro dawa na unaendelea pia katika wilaya za Mpanda, Tanganyika, Mpimbwe, Sumbawanga, Kalambo na Nkasi kwa upande wa Kanda ya Magharibi.

“Huu ni mwendelezo tu wa shughuli zetu za kila siku, kwani Shirika linahakikisha ukaguzi kama huu unafanyika katika kila wilaya nchi nzima ili kuhakikisha tatizo la bidhaa hafifu linapungua kwa kiasi kikubwa kama sio kwisha kabisa,” amesema.

Afisa udhibiti ubora TBS, Emmanuel Mushi amewasisitiza wafanyabiashara wa maduka ya chakula na vipodozi ambao wamefanyiwa ukaguzi na kupewa gharama za malipo na bado hawajalipia gharama za usajili kulipia mara moja ili wapate kibali cha kuuza bidhaa husika katika majengo hayo ili kuepuka usumbufu na wale ambao hawajasajili majengo yao kusajili mara moja.

Meneja wa kiwanda cha kuzalisha maji wilayani Kibondo kijulikanacho kama “Malagarasi Mineral General Supply”, Samir Adam aliipongeza TBS kwa kusogeza huduma karibu na amekuwa akipata ushirikiano wa kutosha kutoka ofisi ya kanda ya magharibi- Kigoma.

Mmiliki wa duka la chakula na vipodozi wilayani Kakonko akionesha kibali chake cha jengo kwa wakaguzi wa TBS wakati wa ukaguzi wa kushtukiza sokoni na usajili wa majengo ya bidhaa za chakula na vipodozi. TBS inawakumbusha wenye majengo hayo kusajili ili kuepuka usumbufu

” Hapo mwanzo tulipoanza tulikuwa na changamoto ya kupata cheti na kutembelewa kwa wakati ila kwa sasa nashukuru ofisi ya TBS Kanda ya Magharibi iko jirani na inanipa ushirikiano mkubwa sana,” amesema.

Pamoja na ukaguzi huo TBS inatumia fursa hiyo ya kukutana na mfanyabiashara mmoja mmoja kuelezea majukumu ya Shirika ikiwa ni pamoja na yale yaliyokuwa yakifanywa na iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania ( TFDA).