October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais wa Shirikisho la Mpira wa kikapu hapa nchini (TPB), Phares Magesa akiweka saini kwenye kitabu cha maombolezo ya Rais mstaafu wa awamu ya tatu Hayati Benjamin William Mkapa, nyumbani kwake masaki.

TBF, PST waomba Mkapa aenziwe kwa ujenzi wa Arena

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

RAIS wa Shirikisho la Mpira wa kikapu hapa nchini (TPB), Phares Magesa , Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Kulipwa (PST), Anthony Rutta pamoja na wadau wengine wa michezo hapa nchini wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kumuenzi Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamini Mkapa kwa kumalizia ujenzi wa uwanja wa ndani wa Taifa (Sports Arena).

Kwa mujibu wa viongozi mbalimbali wa Serikali ambao walipata nafasi ya kumzungumzia Mkapa na mchango alioutoa kwenye Sekta ya michezo walisema kuwa, kiongozi huyo aliweza kutambua umuhimu wa michezo na kuwekeza kwenye viwanja.

Wakitolea mfano wa uwanja wa Taifa ambao aliubuni, ulikuwa ni uwanja changamano ambao unahusisha soka, riadha pamoja na michezo mingine ya ndani ikiwemo kikapu, ngumi, kuongelea na michezo mingine na katika ramani kulikuwa na ramani ambayo ilionesha kutakuw ana uwanja wa ndani wa kisasa.

Awamu ya kwanza ambayo ni ujenzi wa uwanja wa Uwanja Taifa uliokamilika uligharimu dola milioni 53 ambazo ni zaidi ya Sh. bilioni 100 ambazo nusu ya fedha hizoi zilitolewa na Serikali ya China huku ukiingia kwenye orodha ya viwanja 10 vilivyojengwa kwa gharama kubwa barani Afrika pia ni wa saba kwa kuingiza idadi kubwa ya watazamaji .

Magesa ameliambia Majira kuwa, wanatambua umuhimu wa mchango wake mkubwa alioutoa kwenye michezo kwani fedha hizo angeweza kuelekeza kwenye miradi mingine lakini kutokana na mapenzi yake makubwa kweneye michezo aliona bora kurekebisha miundombinu ya michezo na kufanya timu mbalimbali Duniani kuja hapa nchini kwa ajili ya ziara za kimichezo.

Amesema, pia wanatambua mchango mkubwa kwa Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuendelea kuthamini michezo kwani moja na mambo makubwa ambayo wamefanya na wao wanaona kama sehemu ya kumuenzi Mkapa ni
ujenzi wa uwanja wa michezo Dodoma ambao pia utakuwa na uwanja wa ndani.

Pia ametenga bajeti kwa ajili ya kusaidia timu za Taifa katika mashindano mbalimbali ya kimataifa ambao kwetu ni uamuzi mkubwa na tunampongeza rais Magufuli kwa kupita kwenye nyayo zake.

Magesa amesema kuwa, wanaamini kuwa ili kumuenzi Hayati Mkapa basi jitihada zaidi ziongezeke kwani tumemsikia Msemaji wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari , Dkt. Hassan Abbasi akisema watafanya kila liwezekanalo kuhakikisha wanajjenga uwanja wa Ndani wa Taifa wenye hadhi.

“Ni matumaini kuwa, serikali hii ya Awamu ya Tano watatekeleza jambo hili kama walivyoahidi kwani itadhihirisha kuwa wanathamini wana michezo kama alivyofanya rais wa Awamu ya Tatu, Mzee Mkapa alivyotambua miaka ya nyuma, ” amesema Magesa.

Kwa upande wake, Rutta amesema, kifo cha rais Mkapa ni pigo kubwa kwao kwani alionesha ni jinsi gani alivyothamini michezo mara baada ya kukubali ushauri aliyekuwa waziri wake, Juma Kapuya wa kujenga uwanja wa Taifa.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Kulipwa (PST), Anthony Rutta

Amesema kuwa, sasa wanaamini Serikali itafikiria upya ujenzi wa uwanja wa ndani wa Taifa kama sehemu ya kumuenzi kuongozi huyo kutokana na uwanja wa sasa kutokuwa kwenye hali nzuri.

Rutta amesema kuwa, pia wanaamini kuwa ujenzi wa uwnaja huo utawapunguzia kwa kiasi kikubwa gharama ambazo zimesababisha wandaaji wengi wa mapambano kujiweka kando.

“Kwenye ngumi gharama ni kubwa sana kwani kwani kufunga ulingo pekee kunagraribu zaidi ya Sh milioni 1, bado hujakodi viti wala kulipa wafanyakazi hivyo tunaimani kuwa endapo uwanja huu utajengwa basi gharama zitapungua,” amesema Rutta.

Miezi michache iliyopita, TBF na PST waliiomba Serikali kuweka kipaumbele katika ujenzi wa ukumbi wa michezo (Arena) kama walivyoahidi ili kuleta mapinduzi makubwa zaidi ya shughuli za michezo na sanaa hapa nchini.

Lakini pia itakumbukwa, Februari mwaka huu, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe alikuwatana na wawekezaji wa sekta ya Michezo kutoka Misri wanaotarajia kujenga sehemu kubwa ya Michezo mbalimbali (Sports Arena) hapa Nchini.

Lakini pia mwezi uliopita katika uzinduzi wa Albamu ya Msanii Harmonize, Dkt. Mwakyembe aliweka wazi mpango wa Serikali wa kutaka kujenga ukumbi maalumu wa muziki utakaotumika pia kwa shughuli nyingine za michezo hapa jijini utakaokuwa na uwezo wa kuingiza zaidi ya watu elfu 40.

Kumbi hizo maalum hazitajengwa Dar es Salaam pekee bali hata katika
maeneo mengine ambayo wataona yanafaa kwa kushirikisha sekta binafsi.

Lakini ongezeko la Bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 hadi kufikia kiasi cha sh. bilioni 40.1 kutoka sh. Bilioni 30.9 kwa mwaka wa fedha uliopita kumewapa matumaini zaidi wadau mbalimbali wa michezo ambao wanatamani kuona mazingira ya miundombinu ya michezo ikiimarika zaidi.

Pia endapo Serikali itafanikiwa kujenga ukumbi huo mapema kama walivyoahidi basi ni wazi nchi itapata manufaa makubwa ikiwemo kupewa uwenyeji wa mashindano mbalimbali kama ilivyo kwa majirani zetu, Rwanda.

Toka nchi hiyo imejenga uwanja wa Kigali Arena wameweza kupata uwenyeji wa mashindano mbalimbali makubwa ikiwemo ya mchezo wa kikapu baada ya kuwewa uwenyeji wa mashindano ya Kikapu ya Afrika, nusu fainali na fainali za mashindano yanayosimamiwa na NBA , mashindano ya ya kikapu ya ‘Giants of Africa’ na mengine mengi.