February 28, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TBC kuanzisha kipindi maalum msafara wa watumwa kukuza utalii

Na Joyce Kasiki,Dodoma

SHIRIKA la Utangazaji Tanzania (TBC) hivi karibuni ,linatarajia kuanzisha  kipindi maalum kuhusiana na msafara wa watumwa  kupitia Tanzania Safari Channel chenye kuelezea historia ya njia zilizotumiwa na watumwa kusafirisha mizigo ya wakoloni kutoka Zanzibar kupitia Bagamoyo hadi Ujiji mkoani Tabora.

Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt. Ayoub Rioba, amesema kuwa utafiti wa kina uliofanywa kwa kushirikiana na wataalamu wa historia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) umebaini kuwa njia hii ya kihistoria bado inapitika kwa aina mbalimbali za usafiri kama vile miguu, baiskeli, pikipiki na magari.

Amesema,hatua hiyo  inalenga kuvutia watalii wa ndani na nje ya nchi kutembelea maeneo hayo yenye historia ya kipekee huku akielezea kuwa hiyo ni katika juhudi za kukuza utalii wa kihistoria nchini

“Njia hii ya kihistoria siyo tu inatoa fursa ya kujifunza kuhusu historia ya watumwa, bali pia inatoa nafasi ya kufurahia mandhari ya kipekee ya Tanzania. Hii ni moja ya juhudi za kufanikisha maono ya Rais Samia Suluhu Hassan kupitia kampeni ya Tanzania Royal Tour,” amesema Dkt. Rioba na kuongeza kuwa 

“Njia hii ya kati inaanzia Ujiji mkoani Tabora, ambako watumwa walibebeshwa mizigo ya meno ya tembo na kupelekwa Bagamoyo kabla ya kusafirishwa kwa mashua kwenda Zanzibar. Alama za kihistoria kama majengo ya kale, miti iliyotumika kupumzikia na kunyongea watumwa, bado zinapatikana katika baadhi ya maeneo ya njia hiyo.”

Kuhusu utunzaji wa maeneo hayo ya historia Dkt. Rioba amesema kipindi hiko kitasaidia kizazi cha sasa na vijavyo kujifunza mambo yaliyotokea kipindi cha historia nakutokuruhusu kurudi kwenye utumwa.

Mtaalamu wa historia kutoka UDSM, Salvatory Nyanto, alisema  kuwa kulikuwa na njia tatu kuu za biashara ya watumwa nchini Tanzania—njia ya kati (Tabora hadi Zanzibar), njia ya kusini (Kilwa hadi Mauritius kupitia Zanzibar), na njia ya kaskazini (Tanga kupitia Pangani hadi kwa Wamaasai).

“Hii ni hatua muhimu kwa TBC katika kuendeleza urithi wa kihistoria wa Tanzania na kuhamasisha utalii unaoendana na kuhifadhi kumbukumbu za historia ya nchi.”amesisitiza