Na Mwandishi wetu Timesmajira online
WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) imesema hadi kufikia Octoba 31 mwaka huu inadai zaidi ya billioni 7.8 za kodi ya pango kutoka kwa wapangaji wa nyumba huku billioni 3.5 ni madeni ya taasisi mbalimbali za Serikali.
Kutokana na kudai madeni hayo TBA imesema imeazimia kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wapangaji wote wanaodaiwa kwa kutumia dalali wa Mahakama.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam Novemba 22 mwaka huu Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch Daud Kondoro amesema moja ya hatua TBA itakazochukua ni pamoja na kuwaondoa wadaiwa sugu kwa nguvu kupitia dalali wa Mahakama Wins Auction Mart.
Amesema kwa muda mrefu kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya wapangaji wa nyumba za TBA kutolipa kodi ya pango kwa wakati hali inayosababisha kuwa na malimbikizo makubwa ya madeni huku baadhi wakiamini nyumba hizo ni mali ya umma hivyo hawawezi kutolewa hata wakiwa na madeni makubwa.
“Hali hii imekuwa kikwazo katika juhudi za kutekeleza mipango yetu ya maendeleo kama kufanya ukarabati wa nyumba zilizopo na kujenga nyumba mpya ambazo zitapangishwa au kuuzwa kwa watumishi wa umma,”amesema Arch Kondoro.
Akitaja mikoa inayoongoza kwa madeni hayo ni pamoja na Dodoma, Arusha,Mwanza na Mbeya ambapo deni kubwa la kodi ya pango ni bilioni 1.4.
Arch Kondoro amesema tayari kampuni ya udalali wa Mahakama iitwayo Wins Auction Mart imeshakabidhiwa orodha ya wadaiwa wote kwa ajili ya utekelezaji wa zoezi la kuwaondoa na hatua hiyo itaanza Desemba Mosi, mwaka huu, kwa nchi nzima.
“Hatua itakayofuata baada ya kuwaondoa katika nyumba hizo ni kuwafungulia kesi za madai mahakamani wadaiwa hao ili kuhakikisha wanalipa madeni hayo licha ya kuwa wameshaondolewa katika majengo ya TBA”amesema Arch Kondoro.
Aidha amewataka wapangaji wote zikiwemo taasisi za umma,kuhakikisha wanalipa madeni hayo kwa wakati baada ya kupokea namba za kumbukumbu za malipo ambazo hutumwa kwao kila mwezi kwa njia ya ujumbe mfupi wa
maandishi.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua