December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAWA yawaingiza bil. 4.4 warina asali

Na Christina Cosmas, TimesMajira Online, Morogoro

MAMLAKA ya usimamizi wa wanyamapori Tanzania (TAWA) imewaingizia wananchi kiasi cha shilingi bil 4.4 kutoka kwenye mauzo ya asali kwa kipindi cha miaka minne baada ya kuvielimisha vikundi 58 vya warina asali wanaoishi kandokando ya maeneo ya uhifadhi kwenye mapori ya akiba nchini.

Mapori hayo ya akiba ni pamoja na pori la Ugala, Myuwosi, Rukwa -Rwafu yaliyopo hapa nchini na kwamba fedha hizo zimetokana na mauzo ya asali kutoka kwenye mapori hayo yanayorina asali baada ya kupewa elimu na TAWA.

Kaimu Kamishna wa Uhifadhi kutoka TAWA, Mabula Nyanda amesema, kufuatia kuanzishwa kwa miradi ya kihifadhi ikiwemo ufugaji nyuki kwenye mapori hayo ili kuzuia suala la wanyamapori kuzagaa na kuleta usumbufu kwa jamii, wameamua kuunda na kuviwezesha vikundi hivyo 58 vyenye wanachama 2,068 ili washirikiane nao na kuwa wahifadhi bora baada ya kuona faida ya uhifadhi.

Amesema, TAWA baada ya kutoa elimu wametoa mizinga ya nyuki ipatayo 100,000 kwa wana vikundi hao ambapo katika mavuno ya miaka minne wameweza kuvuna tani 1,000 za asali na kuzalisha kiasi hicho cha fedha shilingi bil 4.4 baada ya mauzo.

“Wananchi wanapaswa kupewa ushirikiano wa kutosha katika kufanya usimamizi shirikishi wa misitu wakiona faida ya misitu suala ambalo tumeanza kulifanya kwa sasa,” amesema Nyanda.