December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaombwa kuzindua chanjo za mifugo

Na Queen Lema, TimesMajira Online , Arusha

Chama cha madaktari wa mifugo wasaidizi (TAVEPA) kimeiomba serikali kuweza kufanya uzinduzi rasmi wa kitaifa wa chanjo za mifugo ambapo chanjo hizo zitaweza kuwasaidia wafugaji kufuga kwa ubora zaidi.

Hayo yameelezwa jijini Arusha na Katibu mkuu wa chama hicho Bw David Mikaeli Tupa wakati akiongea na wataalamu wa mifugo ambao ni wanachama wa chama hicho mapema jana kwenye mkutano wa 18 unaoendelea Arusha.

David alisema kuwa uwepo wa chanjo za mifugo utaweza kusaidia sana wafugaji kuweza kufuga kwa uhakika kwa kuwa chanjo ni muhimu sana.

Alisema kuwa mbali na wafugaji kuwez kufuga kwa uhakika zaidi pia chanjo hizo zinaweza kutumika kama kinga ya magonjwa hali ambayo nayo itaweza kufanya mifugo kuwa kwenye kiwango bora sana.

“tunaomba uzinduzi wa chanjo uwe wa kitaifa hii itasaidia sana hasa kipindi cha magonjwa kwa kuwa magonjwa yanalipuka bila taarifa hivyo chanjo zikiwepo ni nzuri sana kwa ajili ya mifugo”aliongeza.

Katika hatua nyingine aliongeza kuwa ndani ya mkutano huo wa 18 wataweza kujadili mambo mbalimbali ikiwemo pato la taifa ambalo linatokana na mifugo.

“tutaangalia zaidi mambo mbalimbali ambayo yanasababisha mifugo yetu isiweze kuchangia pato la taifa, kwa kiwango kikubwa na hilo nadhani ni muhimu sana kwa kuwa mifugo ina uwezo mkubwa sana wa kuwa juu hasa kwenye pato la taifa”aliongeza .

Alimalizia kwa kuwataka wananchi kote nchini kuhakikisha kwamba watatumia wataalamu wa mifugo endapo kama wamepata changamoto yoyote ile ikiwa ni pamoja na kutafuta ushauri wa kitaalamu kila mara ili mifugo iweze kufugwa kwa njia ambayo ni ya kisasa na ambayo itaweza kufanya bidhaa ziweze kutok hata nje ya nchi.