January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tatizo la rushwa ya ngono mahali pa kazi linaendelea kushika mizizi

Na Mwandishi wetu,timesmajira,Online

CHAMA cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na Friedrich-Ebert-Stiftung (FES) Tanzania,wamebaini kuwa tatizo la rushwa ya ngono mahala pa kazi linaendelea kushika mizizi katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Akizungumza hayo leo jijini Dar es Salaam,Mkurugenzi wa TAMWA ,Dkt Rose Reuben wakati akizungumza  na waandishi wa habari juu ya kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia amesema tatizo la rushwa ya ngono ni kubwa lakini limegubikwa na ukimya, wahanga wengi hawatoi taarifa wakiogopa kudhalilishwa.


Amesema  rushwa ya ngono vyuoni ndicho chanzo cha kuwa na wanafunzi wasio na tija katika sekta ya ajira, lakini pia ndicho chanzo cha kuzalisha wanaataluma wasio na sifa za kuajiriwa.  “Rushwa hii ya ngono mahala pa kazi na vyuoni, ndicho chanzo pia cha maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na magonjwa mengine ya zinaa,katika tafiti zetu, TAMWA tumegundua kuwa rushwa ya ngono hufanyika sio tu mahala pa kazi, bali wakati mwingine, hata katika kambi za wakimbizi, katika shule za sekondari,” amesema na kuongeza

“Rushwa ya ngono hurudisha nyuma maendeleo ya mtu mmoja mmoja na nchi kwa sababu matokeo ya ukatili wa aina hii ni kurudisha nyuma ari ya utendaji kazi wa wanafunzi, wafanyakazi au waumini, ” amesisitiza Dkt. Reuben


 Aidha amesema wanakemea   vikali ukatili kwa njia ya mtandao unaoendelea kwani wamesikia na wakati mwingine watu wenyewe ndiyo wamekuwa waanzilishi wa ukatili huu. “Kutumia picha za wanawake vibaya, kutumia lugha dhalili kwa kundi fulani mitandaoni, kutumia picha za watoto na kuweka maudhui yanayomdhalilisha haya ni baadhi tu ya matendo yanayochagiza ukatili wa kijinsia mitandaoni,”amesema

 
Kwa upande wake Mkuu wa mradi  wa Taasisi ya FES,Anna Mbise amesema taasisi yao inafanya  shughuli mbalimbali  ikiwemo masuala ya usawa ,demokrasia na masuala ya utawala bora.


Amesema wameshirikiana na TAMWA katika kukemea ukatili wa mitandaoni na ni kampeni ambayo walianza tangu aprili mwaka huu.”Sisi kama shirika tunaangalia masuala ya usawa tunajua kuwa hakuna maendeleo endelevu kama  tutawaacha watu nyuma,kama hakuna usawa hata mitandaoni baadhi ya watu wanafanyiwa ukatili mitandaoni watashindwa kushiriki katika kufanya shughuli zao,” amesema