January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tathimini ya Mpango wa ya Pili wa Kunusuru Kaya Maskini Wazinduliwa Viziwani Zanzibar

Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline, Zanzibar

MAKAMU wa Pili wa Rais ,Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Tanzania inatekeleza Awamu ya Pili ya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (PSSN II) yenye lengo kuzifikia kaya milioni 1.4 katika shehia, vijiji na mitaa yote hapa nchini.

Amesema Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ni mojawapo ya mipango mikubwa inayotekelezwa nchini kwa kushirikisha kaya za walengwa katika kupambana na umaskini na kuimarisha uchumi wao.

Makamu wa Rais Abdulla ameyasema hayo mwishoni mwa wiki (Septemba 21,2024) katika hafla ya Uzinduzi wa Tathimini ya mwisho ya kupima matokeo ya kipindi cha pili cha Mpango wa kunusuru kaya masikini (PSSN II) ya mwaka 2024 .

Amesema kuwa ili kufanikisha malengo ya Mpango yaliyokusudiwa, Mpango unatoa ruzuku ya msingi kwa kaya za walengwa ambazo pia zinapaswa kutimiza masharti ya elimu na afya. Pia, kaya hizi zinanufaika kwa kushiriki katika miradi ya jamii yenye lengo la kutoa fursa za ajira za muda.

“Katika utekelezaji wa mpango wa Kuweka Akiba na Kuwekeza, kaya za walengwa wanapata mafunzo ya stadi za ujasiriamali na mbinu za kuunda vikundi endelevu vya kuweka akiba na kuwekeza.

Vile vile, amesema miradi ya kuendeleza miundombinu ya afya, elimu, barabara, kilimo, mazingira na maji inatekelezwa na walengwa kupitia Mpango huu.

Amesema kupitia Mpango huo, takwimu zinaonesha kuwa, kuanzia mwaka 2000 hadi Mwezi Agosti, 2024, Serikali kupitia Mpango huu imesaidia kaya za walengwa wapatao 1,450,000 (sawa na wastani wa watu 6,960,000). Kati ya kaya hizo kaya 394,500 (sawa na wastani wa watu 1,893,600) tayari zimeshajikomboa kutoka kwenye umaskini uliokithiri.

Amefafanua kuwa Kaya hizo zimehitimu na kutoka katika Mpango baada ya hali zao za maisha kuwa bora zaidi ukilinganisha na kabla ya kushiriki katika Mpango

Amesema Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali (OCGS) Zanzibar na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ndio zenye jukumu la kusimamia takwimu rasmi hapa nchini.hivyo basi, kutokana na uwezo, weledi na umahiri wa Ofisi zetu hizi mbili, Serikali imezipa jukumu la kufanya Tathmini hiyo

“Tathmini hii ina Awamu Mbili ambapo Awamu ya Awali ilifanyika Mwaka 2022 na hii Awamu ya Mwisho inafanyika huu Mwaka wa 2024.”Amesema

Ameongeza kuwa jumla ya mikoa 17 yaani mikoa 14 Tanzania Bara na mikoa 3 Zanzibar yenye jumla ya shehia, vijiji na mitaa 434 itatembelewa kwa ajili ya Tathmini hii. Kati ya hiyo, vijiji na mitaa 376 ni kutoka Tanzania Bara na shehia 58 ni kutoka Zanzibar.

“Madhumuni ya Tathmini hii ni kuweza kupima endapo Mpango huu unafikia malengo yaliyokusudiwa ya kuondoa umaskini kwa kaya zilizoainishwa kuishi katika umaskini uliokithiri.”

Nakuongeza kuwa; ” Tathmini kama hizi hufanyika katika nchi mbalimbali zinazotekeleza mipango kama hii duniani kupitia taasisi za fedha na maendeleo za kimataifa. Katika nchi yetu, Mpango huu unahusisha mikakati zaidi ya mmoja katika utekelezaji ili kuhakikisha kwamba walengwa wanafaidika na kutoka katika hali ya umasikini mapema zaidi.

Hivyo basi, ni matarajio yangu kwamba, Tathmini hii itaweza kutoa taswira halisi ya hali ilivyo na kuiwezesha Serikali kuona ni eneo lipi tunafanya vizuri zaidi na eneo lipi linahitaji kuongeza mkazo. Kama ulivyokuwa kwa Tathmini ya Awali, Serikali inapenda kuona Tathmini ya Mwisho itatupatia takwimu zenye ubora zitakazotuonesha mwenendo wa viashiria mbalimbali vya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini nchini.

Amesema anatambua kuwa Tathmini hiyo inahusisha kukusanya taarifa nyingi ili kujua hali na mwenendo wa umaskini kwa wananchi nakwamba taarifa hizi ni pamoja na za elimu; afya; uwezeshaji wa wanawake; matumizi na usalama wa chakula; namna ya kukabiliana na majanga katika kaya; makazi na rasilimali za kaya

Zingine ni shughuli za kaya zisizokuwa za kilimo; akiba na mikopo; ajira na matumizi ya muda; shughuli za kilimo na mifugo; na unyanyasaji wa kijinsia. Taarifa hizi zote ni muhimu sana katika kutoa viashiria vya hali ya umaskini katika kaya.

Amesema kuwa matokeo ya Tathmini hiyo yanalenga kuonyesha ulinganifu wa hali za kaya zilizomo katika Mpango na unafuu wa gharama za kutekeleza shughuli za Mpango katika shehia, vijiji na mitaa ilivyochaguliwa na ambayo kwa sasa inaendelea kupatiwa fedha za ruzuku kwa walengwa.

Pia matokeo ya Tathmini yanalenga kuonesha mwenendo wa utekelezaji wa shughuli za Mpango huu na kuelekeza maamuzi bora ya kisera ya kuboresha maisha ya kaya maskini nchini.

“Napenda kuzipongeza Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kutekeleza vyema zoezi hili tangu maandalizi hadi kufikia siku ya leo ya uzinduzi.”amesema

Amefafanua kuwa mchakato wa kufanya tafiti linakuwa si rahisi lakini kutokana na umahiri wenu mmeweza kufanya kazi hii ya maandalizi na kuikamilisha kwa wakati kama ilivyopangwa.

Pia amesema anazipongeza Benki ya Dunia na TASAF kwa ushirikiano wao mkubwa wa kiufundi na kutoa miongozo mbalimbali wakati wote wa maandalizi ya shughuli hii. Hongereni sana! Ndugu Washiriki;Nimearifiwa kwamba, Wasimamizi na Wadadisi wa Tathmini hii wametapatiwa mafunzo kwa njia ya nadharia na kwa vitendo, na kujifunza kutumia ‘tablets’.

Ni matarajio yangu kuwa mmeweka jitihada ya kutosha katika kufuatilia mafunzo mliyopewa na Wakufunzi wenu ambayo yatapelekea kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu wa hali ya juu ili lengo la Tathmini hii ifanikiwe na Kumbukeni kuwa Taifa linawategemea sana katika kazi hii.

“Napenda kutoa wito kwa Watendaji wa Serikali na Wananchi kwa ujumla kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Wasimamizi na Wadadisi watakapokuwa katika zoezi hili, ili kazi hii ifanyike bila matatizo yoyote na kwa ufanisi mkubwa.

Kwa namna ya pekee nawaomba Wakuu wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Viongozi na Watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mameneja Takwimu wa Mikoa na viongozi wa shehia, vijiji na mitaa kwa pamoja watoe ushirikiano wa hali ya juu kwa Wasimamizi na Wadadisi watakapokuwa katika maeneo yao kukusanya taarifa za Tathmini hii.”Amesema

” Nina imani kuwa, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar na Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania kwa kushirikiana na TASAF imeshawasiliana na Watendaji Wakuu katika ngazi za Mikoa, Wilaya na Halmashauri kuhusu uwepo wa zoezi hili na malengo yake ili iwe rahisi kwa timu zinazotembelea maeneo yao kupata ushirikiano mkubwa wakati wa utekelezaji wa kazi hii. “Amesisitiza

Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kuhakikisha kuwa kazi hiyo inafanyika kwa mafanikio

Pia ameishukuru Benki ya Dunia kwa kutoa fedha na ushauri; Wadau wengine wa Maendeleo pia kwa kutoa rasilimali fedha pamoja na ushauri; na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuweka mazingira bora ili kuhakikisha Tathmini hii inafanyika kwa mafanikio.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Shedrack Mziray ,akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo amesema PSSN II ilizinduliwa Mwezi Februari 2020, ukhudumia kaya milioni I.4 zenye zaidi ya kaya milioni 6 na utekelezaji wake unafanyika katika vijiji, mitaa na shehia zote nchini.

Amesema madhumuni ya PSSN II ni kuwezesha kaya za walengwa kutumia fursa za kuongeza kipato, huduma za jamii na kuwekeza katika kuendeleza rasilimali watu hususan watoto,” amesema.

Mziray amesema katika kipindi cha kuanzia Julai 2021 hadi Juni 2024, Mpango umehawilisha ruzuku ya zaidi ya Sh. bilioni 945.5 kwa kaya za walengwa.

Amesema TASAF inatekeleza Mpango wa Kutoa Ajira za Muda (PWP) kwa kaya za walengwa, ambapo kwa kipindi hiki jumla ya miradi 27,863 iliibuliwa na wananchi na kutekelezwa na walengwa wa mpango na kiasi cha Sh.bilioni 117.3 kulipa ujira kwa kaya za walengwa 662,374 kwa kushiriki katika kutekeleza miradi.

Mkurugenzi huyo amesema miradi hiyo ilikuwa inahusu kutengeneza miundombinu yenye faida kwa jamii nzima kama miradi ya umwagiliaji, upandaji miti, mabwawa, utunzaji wa ardhi, na barabara zinazounganisha vijiji, mitaa au shehia na barabara kuu.

Mziray amesema pia katika kukuza uchumi wa kaya hadi Juni 2024 kulikuwa na jumla ya vikundi 60,342 vyenye wanachama 838,241, kati ya wanachama hao, wanawake ni 716,515 sawa na asilimia 84.5 na wanaume ni 121,726 asilimia 14.5.

Amesema vikundi hivyo vimekusanya akiba ya Sh bilioni 7.9 na kukopeshana Sh bilioni 3.2 kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza miradi inayowaongezea kipato, huku kaya 84,674 zikipewa mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa biashara na kupatiwa ruzuku ya kuanzisha shughuli za kiuchumi yenye thamani ya Sh bilioni 31.3 hadi kufikia Juni 2024.9.21

Kwaupande wake Mtakwimu mkuu wa Serikali ,Salum Kassim Ali amesema kuwa anaishukuru Ofisi ya TASAF kwa
kuendelea kuziamini Ofisi za Takwimu katika jukumu la kusimamia tafiti hizi.

“Napenda kukuhakikishia kuwa,wadadisi wa zoezi hili wana weledi wa kutosha katika ukusanyaji wa taarifa hizi na kazi hii tutaitekeleza Kwa kiwango kikubwa kabisa na katika ubora unaokubalika.

Pia Mtakwimu Salum ameishukuru Benki ya Dunia na wadau wengine
ambao wamekuwa bega kwa bega na Serikali katika utekelezaji wa
Tathmini hizo