December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja

Na Daud Magesa na Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

KAMPUNI ya Meli Tanzania (TASHICO),imefafanua tukio
la meli ya Mv.Serengeti,kuegemea upande wa nyuma na kutitia chini ndani ya Ziwa
Victoria,katika maegesho ya Bandari ya Mwanza Kusini,Wilaya ya Nyamagana,jijini
Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari Desemba 27,2024,Kaimu Mkurugenzi
Mtendaji wa TASHICO,Wakili Alphonce Paul Sebukoto,amesema Desemba 26, mwaka
huu, majira ya saa 8:00 usiku,meli hiyo ilionekana kulalia upande wa nyuma na
kuzama majini.

Wakili Sebukoto, amesema kilichosababisha meli hiyo ni kuelemewa na maji hakijafahamika,yawezekana kuna chuma kimeoza au kupigwa na mawimbi,hivyo maji yakaingia ndani na kuifanya ielemewe.Itakaponyanyuliwa na kuwekwa sawa na kuondoa maji na kukaguliwa majibu sahihi yatapatikana.

“Tulipata taarifa ya meli kulalia upande wa nyuma,na kuwa maji yanaingia ndani ya meli,ni kweli meli imeingiza maji ikiwa imeegeshwa katika ghati eneo la Bandari ya Mwanza Kusini,”amesema.

Wakili Sebukoto,amesema,meli hiyo iliegeshwa tangu mwaka 2016,ilisitisha kutoa huduma ya usafirishaji wa mizigo na abiria kusubiri kufanyiwa ukarabati mkubwa.

Amesema MV.Serengeti ni miongoni mwa meli nne, zilikuwa hazipo katika uendeshaji ambazo Serikali iliweka mkakati wa kuzifanyia ukarabati mkubwa huku meli nyingine ni MT.Ukerewe, MV. Nyangumi na ML. Wimba,

“MV Serengeti iko katika mpango wa matengenezo mwaka
wa fedha 2024/25,hakuna kizuizi kwa Serikali kutoifanyia ukarabati, ilikuwa inaangaliwa
na wataalamu kiusalama,kutokana na kutofanya kazi,inakaguliwa kila mwaka na imekaguliwa
siku chache ikaonekana iko salama kabla ya kuingiza maji,”amesema.

“Meli hii iliyojengwa mwaka 1988 haijafanya
biashara,ina uwezo wa kubeba abiria 500 na tani 250 za mizigo,ni meli ya faida
kwa TASHICO na Serikali,inaweza kutoa huduma katika maeneo yasiyo na
miundombinu ya bandari hasa visiwani,hivyo tuna umuhimu ya kuikarabati,”.

Aidha,akijibu swali kuhusu tukio hilo pamoja na la Mv. Clarias,amesema ni matukio mawili tofauti,Clarias ililalia upande mmoja
ikiwa imetokea safari katika visiwa vya Gana na Goziba,bado linachunguzwa
likifikia mwisho taarifa itatolewa kama ni uzembe ama hujuma watu watafikishwa
mahakamani.

“Kuhusisha meli na mitambo kutumika inaweza
kusababisha maji kuingia ndani ya meli.MV Clarias stain tube (matundu ya kuruhusu
meli kuingiza maji na kupumua kwa kiwango kinachotakiwa) zilikuwa na upana usio
wa kawaida,hivyo maji kuingia ama kulikuwa na mkono wa mtu,hatua zitachukuliwa
kwa watakaobainika kuhusika,”amesema Wakili Sebukoto.

Amesisitiza usalama ni kipaumbele cha TASHICO,hivyo
katika kudhibiti changamoto zinazojitokeza itaongeza umakini na kuimarisha usalama
ikizingatiwa meli zake zilijengwa zamani bila mifumo ya usalama ya kuhisi matukio
ya hatari.

Naye, Said Sekiboto wa Kitengo cha Uokoaji Ndani ya Maji cha Jeshi la Zimamoto ya Uokoaji, Mkoa wa Mwanza,amesema wanaendelea na
utaratibu wa kuifunga meli katika chombo cha kuinyanyua na kuiweka katika
chelezo.

 “Tulipata taarifa
ya meli kuingiwa maji upande wa nyuma na kuzama,tulifika majira ya saa 8 usiku,hakukuwa
na uwezekano wa kusaidia, hivyo tulirudi kufanya taratibu za kuinyayua,
tukishirikiana na wazamiaji wa Polisi Maji,TPA na TASHICO,”amesema.

Sekiboto amesema vifaa walivyofunga kwenye Chelezo la kunyanyua meli walibaini havikuwa na uwezo,hivyo wameimarisha vifaa hivyo,kuifanya Dock (Chelezo) iinyanyue na kuiibua meli hiyo ambayo imegota hadi
chini upande wa nyuma.

“Meli kwa mbele inaelea na hakuna madhara,isipokuwa nyuma
ilishuka chini sababu ya kuzidiwa na wingi wa maji,tutafyonza maji baada ya
kuinyanyua ili kupunguza maji ya ziwa yaliyoingia ndani ya meli pia,tutamwaga
maji kutoka katika Chelezo,kazi itakayofanyika siku nzima,”amesema.