April 19, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TASHICO yatoa ufafanuzi MV.Victoria kusitisha huduma

Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza

MELI ya MV .Victoria inayomilikiwa na Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO),imepandishwa kwenye chelezo (dry dock) kwa ajili ya kufanya ukaguzi na kubaini changamoto za kiufundi, hasa katika mitambo,sehemu ya juu na chini meli ndani ya maji,ambao utafanyika kwa siku tatu.

Msimamizi wa Usalama wa Meli na Uhifadhi wa Mazingira,Capt.Bembele Ng’wita,amesema hayo jijini Mwanza, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusiana na ukaguzi wa meli hiyo.

Amesema hatua ya ukaguzi huo ni muhimu kwa ajili ya kufanya matengenezo na huduma ya kawaida ili kuhakikisha usalama na ubora wa chombo hicho unaokidhi viwango na sheria za kimataifa.

Capt.Ng’wita amesema “Kufanya ukaguzi wa kina katika maeneo haya kunahakikisha kuwa meli inafanya kazi vizuri na haina matatizo, yanayoweza kusababisha ajali au matatizo ya kiusalama kutokana na baadhi ya vifaa kuchakaa,”.

“Huu ni mchakato wa kawaida katika uendeshaji meli,baada ya kufanya kazi kwa muda mrefu ili kuhakikisha ufanisi na usalama wa safari.Baadhi ya vifaa vinachoka na vinahitaji huduma na ‘ku-legulaty’ chombo kirudi katika hali ya kawaida,”amesema.

Capt.Ng’wita amesema ukaguzi unafanyika katika mitambo, pampu,kangavuke (generator), mifumo ya meli kwa maelekezo ya kiwanda kilichoijenga,vitafungwa vipuri ambavyo tayari vimeagizwa na vimewasili.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano kwa Umma wa TASHICO,Anselem Namala,amesema meli ya MV. Victoria ilisitisha kutoa huduma Machi 4,mwaka huu,kupisha matengenezo ya kawaida baada ya kutoa huduma kwa mwaka,ilifanyiwa ukaguzi wa ndani na juu, kabla ya kupandishwa kwenye chelezo Machi 11,2025.

“MV Victoria Hapa Kazi Tu, kupandishwa kwenye Chelezo kunalenga kufanya ukaguzi wa mwili wa meli inapoelea ili kuangalia maeneo yenye changamoto na kuyarekebisha kabla ya kurejea kutoa huduma ya usafiri na usafirishaji wa mizigo na abiria,”amesema.

Amesema ukaguzi na maboresho hayo,ni hatua muhimu kwa kuzingatia sheria za kimataifa kuhusu usalama wa meli na kuiweka katika hali nzuri kwa ajili ya safari ndefu.