Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Kampuni ya Huduma za Meli(MSCL),imefanya mabadiliko ya jina la kampuni hiyo na sasa inaitwa Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO), ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha sekta ya uchukuzi na huduma za usafiri wa majini, na kujikita katika upanuzi wa biashara katika maeneo ya maziwa makuu na Bahari ya Hindi.
Akitoa taarifa mbele ya Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile, katika uzinduzi wa jina hilo jipya na nembo mpya ya kampuni hiyo,Novemba 18,2024,uliofanyika wilayani Ilemela mkoani Mwanza, Mkurugenzi Mtendaji wa TASHICO, Eric Hamissi,amesema mabadiliko ya jina kutoka Kampuni ya Huduma za Meli Mwanza (MSCL) hadi Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO) ni sehemu ya mikakati ya kupanua huduma za kampuni hiyo na kuongeza ushindani katika soko la ndani na nje ya nchi.
“Tunataka kuakisi vyema shughuli zetu, hasa kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali. Lengo letu ni kuwa na meli kubwa zaidi zinazobeba mizigo, hasa katika Bahari ya Hindi.Tunatarajia kuwa na meli zisizopungua nne katika Bahari ya Hindi ifikapo mwaka 2030,”.
Kwa mujibu wa Hamissi,amesema.kampuni hiyo ilijifufua rasmi mwaka 2015,baada ya kuwa hoi kwa muda mrefu tangu mwaka 2004.Ambapo kupitia ilani ya uchaguzi ya CCM,2015-2020,Serikali ilianza kuwekeza tena katika kampuni hiyo kwa ajili ya kukarabati meli zilizopo na kuongeza uwezo wa kutoa huduma bora.
Hata hivyo,amesema,Serikali imewekeza zaidi ya tirioni 1,katika kuboresha huduma za kampuni hiyo,hivyo wanaendelea kutekeleza miradi ya ujenzi wa meli mpya,ikiwa ni pamoja na meli za abiria na mizigo kwa ajili ya safari za Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika.
“Miradi mingine ni pamoja na ujenzi wa meli zenye uwezo wa kubeba tani 3,000,kwa Ziwa Victoria na tani 3,500 kwa Ziwa Tanganyika,pamoja na kujenga kiwanda cha meli kinachoweza kushughulikia meli,”.
Naibu Waziri wa Uchukuzi,David Kihenzile,amesisitiza kuwa, pamoja na mabadiliko hayo, TASHICO inatakiwa kuongeza ubunifu katika huduma zake, hususani katika usafiri wa abiria na mizigo kupitia meli.
“Tunapoamua kuboresha kampuni yetu ya meli, tunapanua uwezo wa kuhudumia shehena. Rais Samia alifanya juhudi kuimarisha sekta ya usafiri na hivi sasa shehena imeongezeka kutoka tani milioni 5.6 hadi milioni 9,”.
Kihenzile,amesema katika kipindi cha miaka mitatu,Serikali imetoa tirilioni 1.2,kwa ajili ya kuboresha miradi ya meli kwenye maziwa makuu,na Mwanza ni Mkoa muhimu kwa sababu imepakana na nchi jirani kama Kenya, Rwanda, Burundi na Uganda.Hiyo ni hatua muhimu kwa kukuza uchumi wa taifa na kuongeza usafiri wa mizigo.
“Tunapozungumzia uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya usafiri, tunataka kuona fursa nyingi zinazotokana na meli za kisasa.Reli ya Kisasa (SGR) itakapokamilika, idadi ya mizigo inayosafirishwa kupitia njia ya majini itaongezeka,”amesema Kihenzile.
“Uwekezaji mkubwa wa Serikali umetuwezesha kuboresha huduma na kuimarisha huduma za usafiri wa majini. TASHICO sasa ni sura ya kitaifa, na tunashukuru kwa hatua hii ya kukuza biashara zetu,”amesema Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TASHICO, Meja Jenerali mstaafu John Mbungo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Elikana Balandya,amesema, miundombinu ya usafiri ni nguzo muhimu katika maendeleo ya uchumi.Hivyo ametoa ombi kwa Wizara ya Uchukuzi,kuendelea kuzingatia mahitaji ya wananchi, hasa wale wanaotumia usafiri wa majini na reli, ili kuhakikisha huduma zinaboreshwa na kupunguza adha zinazoweza kujitokeza.
Mabadiliko ya jina la TASHICO ni sehemu ya mpango wa kampuni hii kupanua huduma zake na kujitayarisha kushindana kimataifa. Huu ni mwanzo wa hatua kubwa za kibiashara na uchumi zinazolenga kutoa fursa zaidi kwa Watanzania, na kuongeza mchango wa sekta ya uchukuzi katika maendeleo ya taifa.
More Stories
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa
Mgeja aipongeza CCM kwa uteuzi Wagombea Urais