December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TASAF yasomesha watoto wa Kaya Maskini chuo kikuu

Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Tabora

MPANGO wa serikali wa kunusuru kaya maskini kupitia mradi wa TASAF umeleta neema kubwa kwa familia za walengwa katika halmashauri ya manispaa Tabora baada ya kuwakwamua kiuchumi na kusomesha watoto hadi chuo kikuu.

Wakitoa ushuhuda wa manufaa waliyopata kupitia mradi huo mbele ya Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Deus Clement Sangu baadhi ya wanufaika wameshukuru serikali kwa kuleta mradi huo.

Hadija Abdallah Kabutu (52) mkazi wa Mtaa wa Kazaroho, kata ya Mbugani katika halmashauri ya manispaa Tabora ameeleza kuwa kabla ya kuingizwa katika mradi huo alikuwa na hali mbaya sana kiuchumi.

Amebainisha kuwa licha ya kuwa na mume maisha yao yalikuwa tete, hata chakula ilikuwa shida kupata milo 3 hali iliyopelekea watoto wao kushindwa kwenda shule lakini baada ya kuanza kupata fedha za TASAF maisha yao yamebadilika.

‘Nilianza kulima mboga mboga, baadae nikalima mahindi na mpunga, nikivuna nilikuwa nauza kiasi fulani ili kupata fedha na kiasi kingine tunakula hadi sasa nimejenga nyumba nzuri na watoto wangu wote nimewasomesha’, ameeleza.

Bi.Stumai Kassimu (55) mkazi wa Kata ya Ipuli katika manispaa hiyo ameeleza kuwa fedha kidogo anayopata kupitia mradi huo imemwezesha kufanya biashara ndogo ndogo na kufanikiwa kusomesha watoto wake 2 hadi Chuo Kikuu.

‘Tunamshukuru sana Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza mradi huu, kama sio mradi huu watoto wangu wasingefika chuo kikuu, tunaomba mfuko huu uendelee kuwepo, umesaidia maisha ya kaya nyingi zisizo na uwezo’, amesema.

Naye Elizabeth Shaban (30) mkazi wa Mtaa wa Sokoni, Ipuli amesema kuwa baada ya kuingizwa katika mpango huo mwaka 2015 alipewa sh 40,000/- akatumia 30,000 kwa chakula na nguo za watoto na 10,000 akaanzisha mradi wa nyanya.

Amebainisha kuwa mradi huo umeendelea kukua zaidi na sasa anagenge sokoni na anauza vitenge, hali ambayo imemwezesha kusomesha watoto shule ya msingi na mmoja yupo sekondari na sasa ana akiba ya sh 300,000.

Naibu Waziri Sangu amewapongeza kwa kutumia vizuri fedha ya uwezeshwaji wanayopata kwani licha ya kwamba ni kiasi kidogo lakini imekuwa kichochea cha kubadilisha hali zao kiuchumi.

Amesisitiza kuwa serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inajali sana wananchi wake na kuongeza kuwa kwa sasa inakamilisha mpango mwingine wa kuwezesha kaya maskini kupitia miradi shirikishi.