February 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TASAF Korogwe TC yaviasa vikundi vya kuweka na kukopa

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe

VIKUNDI vya Kuweka na Kukopa vilivyowezeshwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Halmashauri ya Mji Korogwe vimetakiwa kuwa endelevu, kwani vikundi hivyo sio VICOBA bali ni kampuni.

Hayo yamesemwa leo Februari 3, 2025 na Afisa Ufuatiliaji wa TASAF (TMO) kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, na Halmashauri ya Mji Korogwe Elizabeth Mwantyala alipokuwa anazungumza na wanufaika wa Mfuko wa TASAF kwenye Mtaa wa Mtonga, Kata ya Mtonga, Halmashauri ya Mji Korogwe.

“Vikundi vyetu sio vya kuvunja, vikundi vyetu ni kampuni. Kampuni haivunjwi kila mwaka. Jiulize yule Bakhresa (Said Salim Bakhresa) ingekuwa kila mwaka unapoanza anaanza upya, angeweza kuwa na hivyo vitu vyote! yaani kila anapoanza mwaka anakuwa mweupe… asingekuwa na kampuni. Hivyo, hauwezi ukafika mbali kwa muundo huo. Muundo wa hivi vikundi vyetu vinatofautiana na vile vikundi vinaitwa VICOBA.

“Nia yako inakuwa ni kuwekeza pesa ndogo ndogo sababu huwezi kupata sh. 50,000 kwa wakati mmoja, lakini baada ya muda unakuwa na sh. 50,000, hivyo inakuwezesha kukopa sh. 150,000 unaweka genge lako la kuuza vitu vidogo vidogo ikiwemo nyanya, vitunguu, mbogamboga na mahitaji mengine ya kila siku ya binadamu. Baada ya muda, na baada ya kuendeleza mtaji wako, utakuwa na mamilioni” alisema Mwantyala.

Mwantyala alisema vikundi hivyo vya kuweka na kukopa vinaweza kuwapa fursa nzuri ya hata kumiliki mabasi ili mradi wawe na shauku ya kuendelea, kwani TASAF Awamu ya Pili iliwahi kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya wajane na makundi mengine maalumu, baadhi ya watu hao walimiliki mpaka mabasi.

“Ukiwa na mtaji una fursa nyingi. Mji wa Korogwe una masoko na magulio mengi, pika uji wako hata kama hauna maziwa, nenda kauze sokoni. Au choma vitumbua vyako, nenda kauze, hata kama wengine watakukopa wewe kubali, kwani wakati wa kurudisha fedha hizo utawaongezea kidogo gharama, hivyo hawatakopa tena bali watakuwa wananunua kwa kutoa fedha cash (taslimu)” alisema Mwantyala.

Mwantyala alilazimika kutoa somo hilo baada ya baadhi ya wanavikundi kueleza kuwa kila ikifika mwishoni mwa mwaka wanavunja vikundi hivyo, na kujinunulia mahitaji kwa ajili ya sikukuu na kuwapeleka watoto shule.

Muwezeshaji wa TASAF Halmashauri ya Mji Korogwe Mohamed Muna ametoa warsha kwa walengwa wa TASAF, Mtaa wa Mtonga kwa kuwataka wanufaika hao kutumia fursa za kuuza nishati safi ya kupikia ikiwemo kuwa mawakala wa kuuza mitungi ya gesi pamoja na majiko yake, walengwa kutumia nishati safi, ambapo itatoa fursa kwao ya kupata muda wa ziada wa kufanya shughuli za kiuchumi na kukuza kipato cha kaya.

Naye Muwezeshaji wa TASAF Halmashauri ya Mji Korogwe Huruka Jumanne akitoa elimu ya nishati safi ya kupikia kwa walengwa wa TASAF Mtaa wa Msambiazi, Kata ya Mtonga alisema waathirika wakubwa wa nishati chafu ya kupikia ni wanawake, hivyo ili kuondokana na madhira hayo, wametakiwa kuacha kutumia nishati chafu ikiwemo kuni, kinyesi cha ng’ombe na mkaa.

Naye muingiza taarifa wa TASAF, Halmashauri ya Mji Korogwe Ramadhan Kipingu aliwaeleza walengwa wa mfuko huo kuwa kwa sasa inatakiwa malipo yao yapitie kwenye simu ama akaunti ya benki. Mpango wa kutoa malipo kwa fedha taslimu upo mbioni kuondolewa kabisa.