December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TARURA yatenga milioni 67 za matengenezo ya barabara

Judith Ferdinand,TimesMajira Online, Mwanza

Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA), Wilaya ya Ilemela kwa mwaka wa fedha wa 2023/24 imetenga kiasi cha zaidi ya milioni 67(67,420,000.00), kwa ajili ya matengenezo ya dharura ya barabara mbalimbali zilizoharibiwa na mvua.

Hayo yamebainishwa na Meneja wa TARURA Wilaya ya Ilemela Mhandisi Sobe Makonyo,wakati alijibu maswali yalioulizwa katika kikao cha Baraza la Madiwani kwa ajili ya kujadili taarifa ya utekelezaji robo ya tatu kipindi cha Januari-Machi,kilichofanyika Mei,15,2023.Ambapo ameeleza kuwa tayari bajeti hiyo imeishapitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Huku kupitia ofisi ya Mbunge TARURA imepokea kiasi cha milioni 15 kwa ajili ya kuchonga barabara mbalimbali zilizoathiriwa na mvua hasa zinazotumiwa na daladala kama vile Buswelu -Nyamadoke-Nyamh’ongolo, Kahama-Isela, Buswelu -Lukobe,Nyafla-Igumamoyo,Mihama-Zahanati na tayari utekelezaji bwa kazi hizo unaendelea.

“Barabara vya Mbogambiga-Nyamadoke-Nyamh’ongolo ni miongoni mwa barabara zilizotengwa kwa ajili ya kuchingwa kwa kutumia fedha za ofisi ya Mbunge na tayari kazi hiyo imeshaanza kutekelezwa ili kuifanya ipitie baada ya kuharibiwa na mvua nyingi zilizonyesha,”ameeleza Mhandisi Sobe.

Sanjari na hayo ameeleza kuwa uwekaji wa alama za barabara na matuta pale inapo bidi katika barabara ya lami ni shughuli za matengy ya barabara zinazofanyika kila mwaka kupitia bajeti za mwaka.

“Katika mwaka wa fedha 2023/24 kiasi cha milioni 120, kimetengwa kwa ajili ya matengenezo hayo ikiwemo na kuziba viraka,”ameeleza Mhandisi Sobe.

Awali Diwani wa Viti Maalum Sara Manyama akiuliza maswali kwa TARURA,alitaka ufafanuzi wa kufahamu kuwa ni lini TARURA itatengeneza barabara ya Sunrise Kata ya Pasiansi ambayo kwa sasa imeharibika na kuwa kero kubwa kwa wananchi.

Pamoja na kuitaka kufahamu mpango wa TARURA wa kutengeneza barabara za mitaa katika halmashauri hiyo ambazo nyingi zimeharibiwa na mvua zilizonyesha kwa kiasi kikubwa.