May 13, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TARURA yapongezwa ukamilishaji miradi kwa wakati

Na Mwandishi wetu,Dar es Salaam

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI)imeupongeza uongozi wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini TARURA kwa kukamilisha miradi kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vya ubora.Hayo yamebainika wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI ilipo kagua miradi inayotekelezwa na TARURA katika Mkoa wa Dar Es Salaam.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa kamati ya TAMISEMI Dennis Londo ameeleza kuwa miradi iliyotembelewa imekamilika kwa wakati na kwa ubora na kwamba itasaidia kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi.” TARURA Mkoa wa Dar Es Salaam wanafanya kazi nzuri, miradi imekamilika kwa wakati na itasaidia kurahisisha shughuli za wananchi kiuchumi na Kijamii” .amesema Londo

Kuhusu Halmashauri zenye mapato ya ndani yanayozidi Billioni tano kutakiwa kuchangia asilimia kumi ya fedha za maendeleo katika ujenzi wa Barabara,Kamati hiyo imeonesha kuridhishwa na Halmashauri za Mkoa wa Dar Salaam kwani tayari zote zimetekeleza agizo hilo la Serikali na tayari zimetoa fedha hizo kwaajili ya ujenzi wa Barabara.

Kwa upande wake Mbunge Salome Makamba ambaye pia ni mjumbe wa Kamati hiyo ameeleza kufurahishwa na kazi zinazofanywa na TARURA huku akitoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanaitunza miundombinu iliyojengwa ili iweze kutumika kwa muda uliokusudiwa.” Kazi iliyofanyika chini ya TARURA ni kubwa lakini niwasihi wananchi kuhakikisha wanaitunza miundombinu hii ili iweze kutumika kwa muda uliokusudiwa na kuleta tija katika nchi kiuchumi na Kijamii”.

Naye Mkurugenzi wa Barabara kutoka TARURA mhandisi Venanti Komba amesema kuwa ushauri wa Kamati hiyo umechukuliwa na utafanyiwa kazi ili kuendelea kuboresha na kuwapatia huduma ya usafiri na usafirishaji wananchi.