November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TARURA yaomba Mkandarasi aitwe

Judith Ferdinand,Mwanza

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini(TARURA),Wilaya ya Ilemela,imemuomba Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kumuita Mkandarasi,anayetekeleza mradi wa ujenzi wa barabara ya Buswelu-Cocacola Km 3.3,ili kutoa ufafanuzi wa jinsi atakavyotekeleza kazi hiyo na kufidia muda uliopotea.

Ombi hilo limetolewa Novemba 6,2024,katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/2025(Julai-Septemba) na Kaimu Meneja TARURA Wilaya ya Ilemela,Mhandisi Gavidas Mlyuka,wakati akijibu swali lililoulizwa na Diwani wa Kata ya Buswelu,Sarah Ng’hwani,aliyetaka kujua lini ujenzi wa barabara ya Buswelu-Cocacola,utakamilika maana mkandarasi ameishalipwa?.

Mhandisi Gavidas,alisema,ujenzi wa barabara ya Buswelu-Cocacola,utekelezaji wake umeishaanza kwa mkandarasi kufanya kazi mbalimbali ikiwemo,kusafisha eneo la ujenzi wa barabara,kuondoa tabaka la juu la udongo dhaifu.Kuhamisha miundombinu ya maji na umeme iliopo katika eneo la mradi huo.

Alisema,mradi huo unapaswa kutekelezwa kwa miezi 13,kuanzia Machi 2024 mpaka Machi,2025,mpaka sasa utekelezaji wake ni asilimia zaidi ya 25,huku Mkandarasi huyo akiwa amelipwa kiasi cha ‘certificate’ tano kati ya saba alizokuwa ameziomba.

“Kasi ya mkadarasi kutekeleza kazi hiyo hairidhishi,kutokana na muda uliotumika ukilinganisha na hatua aliyofikia.TARURA kupitia vikao kazi vya mradi na kwa usimamizi wa Mhandisi Mshauri,imekuwa ikimsisitiza kuongeza kasi ya utekelezaji,lakini mpaka sasa yupo nyuma ya mpango kazi aliouwasilisha.Tunamuomba mwajiri(Mkurugenzi),kumuimkandarasi ili kutoa ufafanuzi wa jinsi atakavyotekeleza kazi hiyo na kufidia muda uliopotea,”.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Ummy Wayayu,alisema ataendelea kufanya mazungumzo na mkandarasi aliyepewa kazi ya kujenga barabara hiyo ili awasikilize wanayapi na kuyapeleka Ofisi ya Rais TAMISEMI.

“Tukisha jadiliana wakaniambia changamoto walizonanzo,zile ambazo zipo ndani ya Halmashauri nitazitatua kwa uwezo wangu, na zilizo nje nitapeleka kwenye Wizara husika kwa ajili ya kutoa ufafanuzi,”alisema Wayayu.