Na Hadija Bagasha Tanga, TimesMajira Online
Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Tanga, wamekabidhi kazi ya kukusanya ushuru wa maegesho ya vyombo vya usafiri (Parking fees) kwa uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga ikiwa ni utekelezaji wa maamuzi ya Serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI iliyotangaza kurudisha ukusanyaji wa ushuru wa maegesho kwa mamlaka ya Serikali za mitaa kuanzia mwaka wa fedha 2022/2023.
Makabidhiano hayo yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa jengo la Ofisi kuu ya Halmashauri ya Jiji la Tanga, ambapo Halmashauri imewakilishwa na Mstahiki Meya Mhe. Abdulrahman Shiloow na TARURA Mkoa wa Tanga ikiwakilishwa na Meneja wa Mkoa Mhandisi George Tarimo.
Viongozi wengine waliohudhuria Makabidhiano hayo ni pamoja na Naibu Meya Mhe. Colyvas Joseph, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji Bw. Jacob Samwel, Meneja wa TARURA Wilaya ya Tanga Mhandisi Boniface Mwambene, baadhi ya Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri na TARURA.
Akiongea wakati wa makabidhiano hayo, Mhandisi Tarimo amesema TARURA wapo tayari kushirikiana na Jiji la Tanga katika kufanikisha kazi ya kukusanya ushuru na kutenga maeneo ya maegesho ya vyombo vya usafiri, huku akishauri watu wa mapato wa Jiji kufanya ufuatiliaji wa karibu kwa wakusanyaji kwani kunahitajika ufuatiliaji na wakati mwingine kwa kushtukuza ili kuhakiki iwapo magari yaliyopo kwenye maegesho yameingizwa kwenye mfumo.
“Katika kukusanya mapato tumekuwa tukitumia mfumo wa TeRMIS (TARURA eREVENUE MANAGEMENT INFORMATION SYSTEM) ambao mnaweza kuurithi kwasasa hadi hapo baadae mtakapoamua muende vipi. Mkurugenzi uteua watu wako waje wakae na watu wetu kuanzia kesho (Ijumaa, Julai mosi), wataelekezana matumizi ya huo mfumo ili kazi ya kukusanya maduhuli ya Serikali isisimame.” Amesema Mhandisi Tarimo.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa jiji hilo Abdulrahmn Shiloo amesema anaamini kazi hiyo itafanyika vizuri kwani sio kitu kigeni kwa Halmashauri kwa kuwa kabla ya kwenda TARURA ilitekelezwa katika ngazi ya Halmashauri.
“Sasa waswahili wanasema, mchuzi wa mbwa hunywewa wa moto, hivyo muandae utaratibu wiki hii, muwaite wale wote waliokuwa wakifanyakazi na TARURA katika kukusanya ushuru wa maegesho, mkae nao mu-update(mhuishe) taarifa zao, na kishe muendelee nao na kazi” Aliagiza Mstahiki Shiloo.
Katika makabidhiano hayo, TARURA imekabidhi mali na vifaa walivyokuwa wakitumia katika kukusanya ushuru wa maegesho zikiwemo mashine za malipo (POS) 42 ambapo kati ya hizo, mashine 15 zilikuwa zikiendelea na kazi mtaani, mashine 10 zilikabidhiwa zikiwa nzima na mashine 17 zikiwa na hitilafu.
TARURA pia imekabidhi wafanyakazi wa ajira ya muda waliokuwa wakifanya kazi hiyo, mfumo wa makusanyo, nakala ya sheria inayotumika na mkataba wa makubaliano (MoU).
Uondoaji wa kazi ya makusanyo ya maegesho (parking fees) kwa TARURA kuna lengo la kuiwezesha kujikita katika jukumu lake la msingi la ujenzi na matengenezo ya barabara na madaraja ya mijini na vijijini.
Katika kufikia azma ya Serikali ya kuhakikisha usafi na usalama wa miji, Ofisi ya Rais TAMISEMI ilitangaza kurejesha kazi ya kukusanya ushuru wa maegesho kwa mamlaka za Serikali za mitaa kuanzia mwaka wa fedha 2022/2023, ili fedha zitakazo kusanywa, sehemu yake zirudi kwenye Halmashauri ziweze kutumika kwa ajili ya kugharamia usafi wa Barabara, mifereji na uwekaji na uendeshaji wa taa za barabarani katika mamlaka husika.
More Stories
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti