March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TARI Kihinga waongeza uzalishaji mbegu bora za Mchikichi

Na Allan Kitwe,Timesmajiraonline,Tabora

KATIKA kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI-Kihinga) imefanikiwa kuongeza uzalishaji wa mbegu bora za michikichi na kuzigawa kwa wakulima katika Mikoa zaidi ya 18.

Mbegu zilizozalishwa na kusambazwa kwa wakulima tangu mwaka 2021 hadi sasa zimefikia milioni 4.7, idadi hii imeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na serikali katika kuboresha sekta hiyo.

Akizungumza na Timesmajira hivi karibuni Mjini hapa, Afisa Uhawilishaji, Teknolojia na Mahusiano wa Taasisi hiyo iliyoko Mkoani Kigoma, Kuzenza Madili Lushinge ameeleza kufurahishwa na mafanikio makubwa waliyopata.

Amesema kuwa awali zao hilo lilikuwa halipewi kipaumbele kikubwa na lilikuwa linalimwa kwa mazoea hali iliyopelekea wakulima kutopata manufaa makubwa, lakini sasa baada ya kufanyiwa utafiti limeongezewa thamani na kupendwa zaidi.

Amefafanua kuwa wataalamu wa TARI Kihinga wameendelea kuongeza ubunifu na kuzalisha mbegu bora za zao hilo ambazo zimeleta neema kubwa kwa wakulima kwa kuzalisha matunda mengi hivyo kuwapa mafuta mengi na bidhaa nyinginezo.

Mbali na mafuta ya mawese yanayozalishwa kwa ajili ya kupikia, ametaja bidhaa nyingine zinazotokana na zao hilo kuwa ni mafuta ya kupaka (vipodozi), sabuni ya maji na ya mche, mbolea ya kurutubisha shamba, mkaa mbadala na nyiginezo.

Lushinge amedokeza kuwa elimu na hamasa inayoendelea kutolewa na wataalamu wa Taasisi hiyo imechochea wananchi wengi zaidi kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini kuchangamkia kilimo cha zao hilo, hivyo kuomba wapelekewe mbegu zaidi.

‘Katika kipindi cha miaka 5 tumefanikiwa kusambaza takribani miche milioni 4 na laki 7 ya mbegu bora za michikichi kwa wakulima wa Mikoa zaidi ya 18 hapa nchini, uhitaji wa mbegu katika Mikoa hiyo bado ni mkubwa’, ameeleza.

Ametaja baadhi ya Mikoa iliyonufaika na mbegu zilizozalishwa katika Kituo hicho kuwa ni Kigoma, Morogoro, Tabora, Pwani, Mbeya, Ruvuma, Mtwara, Tanga, Rukwa, Katavi, Songwe, Kagera, Mwanza, Geita, Lindi na Dar es salaam.

Mikoa mingine ni Zanzibar (Unguja), Dodoma, Arusha na Singida na Mikoa ambayo haijapelekewa mbegu hizo kutokana na uzalishaji kidogo kuwa ni Kilimanjaro, Iringa, Simiyu, Shinyanga, Manyara, Mara na Njombe.