Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Dar es Salaam
UMOJA wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara (TAPSHA) umeazimia kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uboreshaji wa miundombinu katika shule zote nchini.
TAPSHA umetolea mfano maeneo yaliyoboreshwa kuwa ni pamoja na ujenzi wa shule mpya kupitia mradi wa BOOST kila kona nchini, vyoo vya kisasa vya wanafunzi, ukarabati wa vyumba vya madarasa, ununuzi na utengenezaji wa madawati, usambazaji wa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kupitia GPE LANES II na ugawaji wa vishikwambi kwa walimu.
Tamko hilo limetolewa jijini Dar es Salaam na umoja huo kupitia risala iliyosomwa mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ambapo mkutano huo ulibebwa na kauli mbiu isemayo ‘yamewezekana yasiyowezekana katika elimu nchini’,
“Kauli hii inajidhihirisha wazi jinsi Rais Samia Suluhu Hassan anavyowezesha uboreshaji wa miundombinu katika shule zetu kote nchini,” imesema sehemu ya risala hiyo.
Mwenyekiti wa TAPSHA, Wilaya ya Ilala upande wa shule za msingi za serikali, Godrick Rutayungururwa, amesema,waliweka maazimio ya mwaka 2024 na kupeana taarifa za mwaka 2023 ikiwemo azimio la kumpongeza, Rais Samia, kwa jitihada anazozifanya za kuhakikisha elimu nchini inaendelea kwa kuipa kipaumbele kwa ajili ya watoto pamoja na kuhangaikia maslahi ya walimu.
Naye Mwenyekiti wa TAPSHA, upande wa shule za msingi binafsi Jefta Chaulo, amesema wameazimia kumpongeza Rais Samia kwa kazi kubwa anayoifanya katika sekta ya elimu.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewapongeza Walimu Wakuu wa shule za msingi za serikali na binafsi kwa ufaulu ambao katika kipindi cha miaka minne Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inaongoza kitaifa.
“Hata mwaka huu ufaulu umeongezeka kwa kiwango kikubwa mpaka kupata zaidi ya asilimia 97.8 nawapongeza umoja huu kwa usimamizi mzuri wa miradi inayoendelea kutekelezwa katika ngazi za chin,ninawasihi kuna fedha nyingi ambazo Rais anazipeleka katika halmashauri kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mkaisimamie vizuri na lazima itekelezwe kwa ubora unaotakiwa,”amesema.
Mpogolo ameeleza kuwa, walimu wana thamani kubwa kwao kutokana na mafanikio wanayoendelea kuyapata huku akitolea mfano wa Septemba mwaka huu.
“Wakati wa likizo tulikuwa na zoezi la ukusanyaji wa takwimu za wafanyabiashara katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, lakini tuliwatumia walimu kubaini wafanyabiashara ambao walikuwa hawana leseni, waliokuwa na leseni feki na vibali feki,”amesema Mpogolo.
Aidha, amewaomba waendelee kumuunga mkono Mkurgenzi wa jiji la Dar es Salaam, Jomaary Satura, kutokana na jitihada mbalimbali anazozifanya, huku akitolea ufafanuzi wa ongezeko la mapato katika halmashauri hiyo kutoka bilioni 6 hadi bilioni 10 kwa mwezi na ongezeko la kutoka katika makusanyo wanalolitegemea kutoka bilioni 89 kwenda hadi bilioni 120.
“Ninawaomba waendelee kumuunga mkono mkurugenzi huyo kwa kuwa kitendo hicho kimesaidia kwenda kutengeneza viti na meza kwa shule za sekondari 17,600 na madawati kwa shule za msingi 20000 tulikuwa tunatengeneza meza na viti kwa 135,000 hivi sasa tunatengeneza kwa 80,000 kwa maana yake kwa idadi hiyo ya 17,000 tumeweza kuokoa milioni 800,” amesema.
Ameendelea kusema kuwa kwa upande wa madawati ya shule za msingi zamani walikuwa wakitengeneza kwa 150,000, hivi sasa wanatengeneza kwa 110,000 kwa kila dawati, hivyo kuokoa 40,000 na kwa madawati 20,000 wameweza kuokoa milioni 800, ambapo kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya hiyo, halmashauri kwa upande wa madawati, viti na meza imeokoa bilioni 1.6.
Sanjari na hayo ameeleza kuwa Wilaya hiyo imepatiwa zaidi ya bilioni 15 na serikali kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya elimu msingi, kugharamia elimu bure na mitihani, ununuzi wa vitabu vya kiada na ziada na kupelekea ufaulu kufikia 98.7%, huku akisisitiza kuwa Ilala inaazimia kuwa na watoto wote wanaoanza shule wanamaliza na kufaulu.
Hata hivyo umoja huo katika Jiji la Dar es Salaam unaoundwa na walimu 309 kati ya hao walimu wakuu ni 139 wa shule za serikali 170 wa shule zisizo za serikali huku wakifanikiwa kupunguza idadi ya wanafunzi wasiomudu KKK.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi