Na Mwandishi wetu, Timesmajira
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii zimekubaliana kushirikiana na Serikali ya Oman katika sekta ya maliasili na Utalii kwa lengo la kuboresha sekta hiyo.
Hayo yamejiri wakati wa kikao kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii,Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) na Balozi wa Oman nchini Tanzania, Mhe. Saud Al-Shidhani kilichofanyika leo Machi 6,2025 jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika kikao hicho, Chana amesema kuwa ni wakati muafaka kwa nchi hizo mbili kupanua wigo wa ushirikiano kwa kuziunganisha sekta za utalii na ukarimu kwa kusaini Hati za Makubaliano (MoU) katika nyanja mbalimbali ikiwemo uwekezaji na mafunzo.

“Tunahimiza ushirikiano kati ya mashirika ya utalii na usafirishaji kutoka nchi zote mbili, ili kuboresha shughuli za uuzaji na utangazaji wa utalii sambamba na kukuza ushirikiano miongoni mwa wadau wa utalii kutoka pande zote mbili, kama vile waongoza watalii na wamiliki wa hoteli, na kuunda mtandao wa biashara kati ya nchi hizo mbili” Chana amesisitiza.
Aidha Chana amefafanua kuwa nchi hizo mbili zishirikiane katika ushiriki kwenye matukio ya utalii kama vile maonesho na sherehe zinazofanyika katika mataifa yote mawili akitolea mfano wa Onesho la Swahili International Tourism Expo (S!TE) la nchini Tanzania linalondaliwa na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na pia katika kampeni za kimkakati za uuzaji wa utalii katika Maonesho ya Barabarani “Road Shows” na ziara za Safari za mafunzo “FAM Trips.
“Pia ni vyema tukashirikiana katika uendelezaji wa rasilimali watu, kwa kutilia mkazo katika kujenga uwezo katika mafunzo ya utalii na ukarimu miongoni mwa wadau wa utalii kutoka mataifa yote mawili; hapa napendekeza ushirikiano kati ya taasisi za utalii na mafunzo ya ukarimu” ameongeza Chana.

Naye Balozi wa Oman nchini Tanzania,Saud Al-Shidhani, amesema kuwa Oman iko tayari kushirikiana na Tanzania katika kuendeleza maeneo mbalimbali ya utalii hivyo ni vyema nchi hizo zikawa na Hati za Makubaliano (MoU) katika maeneo husika.
“Sisi tuko tayari kushirikiana katika kutangaza utalii kupitia “road shows”, kuleta watu wenye ushawishi kuja hapa Tanzania na kuwekeza katika maeneo mbalimbali yakiwemo maeneo ya hifadhi za misitu, maziwa , maporomoko ya maji n.k” Al-Shidhani amesema yuko tayari kuziunganisha taasisi za Oman zinazohusiana na masuala ya utalii na taasisi za Tanzania akitolea mfano Chuo cha Taifa cha Utalii na Bodi ya Utalii ya Tanzania.
Kikao hicho kimehudhuriwa na baadhi ya watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) na Makumbusho ya Taifa la Tanzania(NMT).
More Stories
Walimu waaswa kutowatenga watoto wenye ulemavu
Watoto yatima 100 wapatiwa bima za afya Rorya
Wasira afanya mazungumzo na Spika wa Jamhuri ya Cuba