November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania,Marekani kuimarisha ushirikiano wa biashara na uwekezaji nchini

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira online,Dodoma

MAWAZIRI wawili wa Wizara za Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo na Wizara ya Uwekezaji Geoffrey Mwambe wamekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Marekani hapa nchini Bw. Donald Wright kwa lengo la kujenga ushirikiano na kushirikishana fursa za uwekezaji zinazopatikana hapa nchini.

Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo akizungumza na wanahabari mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo na Balozi wa Marekani Bw. Donald Wright ambapo wamefanya mazungumzo kuhusu fulsa za uwekezaji hapa nchini

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mazungumzo hayo Waziri ya Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo amesema katika mazungumzo yao wamelenga kukuza biashara na uwekezaji baina ya nchi mbili za Tanzania na Marekani.

“Leo tumekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Marekani hapa nchini Bw. Donald Wright, kuona namna ya kukuza ushirikiano wetu uliopo baina ya nchi hizi mbili, bado tunafursa nyingi na kubwa za wafanyabiashara wetu kutumia fursa hiyo” amesema Prof. Mkumbo.

Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo na Waziri wa Uwekezaji Geoffrey Mwambe wakipitia kitabu chenye fulsa za uwekezaji walivyokabidhiwa na Balozi wa Marekani Bw Donald Wright mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo.

Amesema katika mazungumzo hayo wamekubaliana kuweka jitihada za kuhakikisha nchi hizo mbili zinazidi kushirikiana katika nyanja za kiuwekezaji na kuleta manufaa na kuwawezesha wafanyabiashara kuwanya biashara kukuza uchumi wa nchi na mtu mmoja moja.

Amesema katika mazungumzo hayo pia wamezungumzia kuhusu mazao ya kimkakati hasa katika kuchakata na sio kuuza malighafi, na hatimaye mazao hayo yachakatwe hapa nchini na kuuza bidhaa badala ya kuuza malighafi, na sekta ya matunda ambayo yanapatikana kwa wingi hapa nchini.

Naye Waziri wa Uwekezaji Geoffrey Mwambe amesema katika mazungumzo hayo pia wamezungumza kuhusu uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwamo ya afya hapa nchini, na wameonekana kuridhika na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika uwekezaji.

Balozi wa Marekani Bw.Donald Wright akimkabidhi kitabu Waziri wa Uwekezaji kinachoonesha fursa mbalimbali zinazohitajika kuwekeza, mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo yao yaliyofanyika jana jijini Dodoma,kulia ni Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Prof.Kitila Mkumbo akionyesha kitabu hicho.

Amesema wawekezaji kutoka Marekani wameonyesha wapo tayari kuja kuwekeza hapa nchini ambapo tayari kuna kampuni imeonyesha nia ya kuja kuwekeza katika sekta ya mawasiliano kwa kuwekeza katika kampuni ya simu, na kampuni ya utalii kutoka Arusha imeonyesha nia ya kutaka kuongeza zaidi uwekezaji.

“Tumeongelea uchakataji wa mazao na ukiangalia Marekani ananunua korosho nchi flani, na ukiangalia sisi tunauza korosho ghafi na hizo nchi zinachakata na kuuza marekani, na sisi sasa tunaweza kuzichakata hapa nchini na kuuza Marekani” amesema Waziri Mwambe.

Amesema pia yapo mazao mengine ya kumkakati kama Kahawa na Pamba ambayo yatachakatwa na kuuzwa nje ya nchi hatimaye kama nchi kupata mapato kupitia kodi na kukuza ajira kwa wananchi ambao watapata ajira katika viwanda hivyo vitakavyoanzishwa.

Amesema katika mazungumzo hayo wamekubaliana kufanya majadiliano mara kwa mara ili kuuisha makubaliano yao ambapo watakuwa wakifanya tathmini kuona makubaliano hayo yanavyofanya kazi katika kuimarisha ushirikiano uliopo kwa miaka sitini sasa baina ya haya mataifa mawili.

Kwa upande wake Balozi wa marekani nchini Tanzania Donald J. Wright amefurahishwa na ushirikiano wa kudumu wa Zaidi ya miaka 70 uliopo kati ya Tanzania na Marekani na

Wright ameahidi kuwa Serikali ya Marekani itashirikiana kwa dhati na kwa karibu na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha wawekezaji kutoka marekani wanakuja kuwekeza nchini Tanzania kwani nchi hii ina fursa nyingi za uwekezaji pamoja na hali nzuri ya ulinzi na usalama.

Balozi Wright amesema kuwa Marekani imetengeneza historia kubwa katika kusaidia maendeleo ya Tanzania katika miradi ya kupambana na magonjwa, Ulinzi, elimu, miundombinu n.k ambapo hiyo imepelekea uhusiano kati ya Marekani na Tanzania kuimarika zaidi.