December 12, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania,EU kushirikiana katika kufanya utafiti wa kina wa madini

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yaahidi kuendelea kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) katika kufanya utafiti wa kina utakaosaidia kupata taarifa sahihi za maeneo madini yanapopatikana ili kuongeza uwekezaji katika uvunaji rasilimali madini hususani madini mkakati kwa manufaa na maslahi ya Watanzania.

Hayo yamesemwa leo Desemba 11 Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde alipokutana na ujumbe wa uwakilishi kutoka EU ukiongozwa na Hanspaul Stausboll ambaye ni Mkurugenzi wa Miradi ya EU Bara la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

“Utafiti ni moyo wa sekta ya madini, na ndiyo maana Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka kipaumbele katika utafiti wa kina wa madini kupitia mkakati kabambe ujulikanao kama Vision 2030 ambao umelenga kuongeza eneo la utafiti kutoka asilimia 16 ya sasa mpaka asilimia 50 ifikapo mwaka 2030. Ni dhahiri kazi hii ni kubwa na Serikali haiwezi kuifanya peke yake pasipo wadau”amesema Mavunde.

“Taarifa njema ni kwamba tayari Serikali tumeshaanza kufanya kazi na EU katika utafiti kupitia Ubalozi wa Hispania nchini. Yapo maeneo ambayo tumeyatambua kwa ajili ya mradi wa kufanya utafiti wa kina wa kurusha ndege na tupo katika hatua za mwisho za kuanza kwa mradi huo wenye manufaa makubwa kwa Nchi yetu ameongeza Waziri Mavunde.

Aidha, Waziri Mavunde amebainisha kwamba mazungumzo hayo na ujumbe wa EU yamejikita katika kuimarisha mashirikiano kwenye uendelezaji sekta ya madini huku ikichagizwa na ukweli kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi chache ulimwenguni zilizobarikiwa madini mbalimbali yakiwemo ya kimkakati kama graphite ambayo ni kivutio kwa wawekezaji wengi kutokana na mwelekeo wa dunia katika kupunguza hewa ukaa ifikapo 2050 kwa matumizi ya nishati safi.

“Eneo la pili tulilozungumza ni eneo la kuyaongezea thamani madini yetu ndani ya nchi badala ya kusafirisha yakiwa ghafi ambapo Nchi tunapoteza mapato, ajira na ustawi wa watanzania. Haya ndio maagizo ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kutaka viwanda vya kuongeza thamani madini kujengwa nchini, hili pia limesisitizwa na Sera yetu ya madini” amesisitiza Mavunde.

Amesema, miradi mbalimba inaendelea kufanyika nchini ikiwemo mradi mkubwa unaojengwa Ngara, mkoani Kagera wa Nikel ikihusisha Kampuni ya Tembo Nickel ambayo Serikali ni mbia. Kupitia mradi huo wa Nikeli ambapo Kampuni kubwa ya BHP anaingia kama mwekezaji, kinakwenda kujengwa kiwanda kikubwa cha usafishaji wa madini ya metali pale Kahama kwenye eneo la Buzwagi Special Economic Zone ambacho kitakuwa na thamani ya zaidi ya Dola Milioni 500.

Vilevile, Waziri Mavunde ameeleza fursa iliyopo katika mradi wa vijana na wanawake kwenye sekta ya madini ujulikanao kama Mining for Brighter Tommorow (MBT) na kutoa rai kwa EU kutoa ushirikiano zaidi katika programu hiyo ili iweze kuleta tija katika kufikia uchumi wa kati wa juu na kuongeza pato la Mtanzania mara mbili ya ilivyo sasa ifikapo kama malengo ya Dira ya Maendeleo 2050 ilivyoeleza.

Naye, Mkurugenzi wa Miradi wa EU kwa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Hanspaul Stausboll ameonesha kufurahishwa na hatua ambazo Serikali inazichukua katika uendelezaji wa sekta ya madini na kusisitiza kwamba EU ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kipaumbele ikiwemo utafiti, ujenzi wa miundombinu katika maeneo ya migodi na mafunzo kwa vitendo ili kuongeza ujuzi kwa Watanzania.