November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania yatafuta muarobaini wa magonjwa yasiyoambukiza

Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online,Dar

SERIKALI imewakusanya watafiti na wataalamu wa afya nchini ili kujadili na kutoka na suluhisho la nini kifanyike ili kukabiliana na Magonjwa Yasiyoambukiza (NCD) ambayo kwa sasa yanatishia maisha ya Watanzania wengi.

Waziri wa Afya, Usatawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt Doroth Gwajima amebainisha hayo wakati akifungua mkutano wa kwanza wa meza ya majadiliano uliofanyika katika katika Chuo Kikuu cha Sayanzi na Afya ya Jamii (MUHAS).

Ameelezea NCD na COVID 19 ni sawa na dada na kaka kwa kuwa kwa sasa ndiyo yanayolisumbua taifa na hata kusababisha Serikali na wadau mbalimbali kutumia fedha nyingi kukabiliana nayo.

“Kuongezeka kwa magonjwa mengine kama Covid 19 kunachangia NCD kuongezeka na hali kuwa mbaya zaidi nchini. Magonjwa hayo yanachukua sehemu kubwa ya bajeti kwani Serikali inakuwa na mizigo miwili hivyo kushindwa kuimudu,” amesema Dkt. Gwajima.

Amesema umefika wakati watafiti, wataalamu wa afya pamoja na wadau wa sekta hiyo kuangalia ni njia gani rahisi na zitakazotumia fedha kidogo ili kukabiliana na magonjwa hayo.

Amesema sehemu kubwa ya bajeti ya Wizara ya Afya hutumika kukabili NCD, lakini kiwango hicho hakitoshi kuleta matokeo chanya kutokana na ukubwa watatizo hilo hapa nchini.

Amesema hali hiyo ndiyo imewasukuma wataalam wa afya pamoja na wadau wa afya nchini kukutana kwa majadiliano ili kuja mbinu zitakazoisaidia Serikali kupitia watunga sera kubuni njia rahisi zitakazotumia fedha kidogo kukabiliana na tatizo hilo.

“Sasa tunawaambia wataalam wetu wajadili namna ya kutumia fedha kidogo kuyakabili magonjwa hayo,” amesema Dkt. Gwajima huku akiwataka kubuni mbinu zitakazosaidia kupata vyanzo vya fedha ili kuiwezesha Serikali kupunguza kuwategemea wafadhili kutoka nje wakati wote.

Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt Doroth Gwajima akifungua mkutano wa meza ya majadiliano uliowahusisha watafiti, wataalamu na wadau wa afya kwa lengo la kutatua changamoto za kifedha katika kukabiliana na Magonjwa Yasiyoambukiza (NCD). Mkutano huo uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Afya ya Jamii Muhimbili (MUHAS). Kutoka kushoto, mbele ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya magonjwa Yasiiyoambukiza (TANCDA), Profesa Andrew Chenge na Katibu wake, Dkt. Kaushik Romaia. Picha na mpigapicha wetu.

Waziri amesema takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa asilimia 33 ya watanzania wanaugua NCD na kwamba tawimu hizi zinaashiria kuwa tatizo ni kubwa na ni tishio kwa maisha ya Watanzania.

Ameelezea takwimu hizo zinaonesha kuwa uwezekano wa Watanzania wenye umri kati ya 30 na 70 kufa kwa NCD ni asilimia 16. Miongoni mwa NCD ni kama vile magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, kisukari, saratani, matatizo ya figo na ubongo.

Amesema ukubwa wa tatizo hilo pia umekuwa ukichangiwa na uwepo wa magonjwa mengine ya kuambukiza kama vile Virusi Vya Ukimwi (VVU), malaria na kifua kikuu.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wataalam wa afya, watafiti , watoa huduma za afya, kampuni za bima, wadau wa maendeleo, taasisi za fedha na mashirika yasiyo ya kiserikali.

Katika hatua nyingine, Dkt Gwajima amewataka wataalamu hao kutafsiri maazimio watakayofikia katika lugha rahisi ili yaweze kueleweka vyama kwa wananchi.

“Nawaomba sana hili jambo mlichukulie kwa umakini na kuhakikisha yote mtakayofikia muyatafsiri kwa lugha rahisi ambayo itawezesha wananchi kuyaelewa kwa urahisi,” amesema Dkt. Gwajima akibainisha kuwa wataalamu wengi nchini hupenda kutoa taarifa zao kwa lugha ya Kiingereza jambo ambalo linaweza kuwa gumu kueleweka kwa sababu Watanzania wengi wanaelewa zaidi Kiswahili.